Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia imeilalamikia Serikali baada ya mmoja wa viongozi wake kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kunyang’anywa hati ya kusafiria.
Taarifa ya Acacia iliyotolewa jana imeeleza kuwa bosi huyo, ambaye ni mwajiriwa wa mgodi wa Pangea, si raia wa Tanzania na baada ya kukamatwa alishikiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa.
“Baada ya mgongano wa kisheria, bosi huyo aliruhusiwa na akarudishiwa pasipoti yake,” inasema taarifa hiyo.
Acacia, ambayo ina mgogoro na Serikali kuhusu taarifa za kiwango cha dhahabu kilichomo kwenye makinikia, imesema kukamatwa kwa bosi huyo ni miongoni mwa mfululizo wa matukio ya kubughudhiwa kwa wafanyakazi wake na vyombo vya Serikali katika siku mbili zilizopita.
“Acacia inafanya kazi na washauri wetu wa kisheria na mamlaka nyingine ili kuwalinda watu wetu,” inasema taarifa hiyo.
Hata hivyo, kamanda wa polisi wa Uwanja vya Ndege, Martin Otieno alisema hana taarifa za kukamatwa kwa kiongozi yeyote wa Acacia.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Acacia inafanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi na inalipa kodi zote na mrabaha kama sheria inavyosema.
Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliipelekea Acacia makisio ya kodi ya Sh404 trilioni, kiwango ambacho kampuni hiyo imekipinga.
Serikali inadai kuwa Acacia haikusema ukweli kuhusu kiwango cha madini kilichomo kwenye mchanga unaosafirishwa nje.







No comments:
Post a Comment