Wakati kuna vilio kila kona nchini na sehemu mbalimbali duniani kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri maisha ya watu, wanyama na viumbe hai vingine, hatari kubwa inatabiriwa kuwapo nchini iwapo hatua hazitachukulia kukabiliana na hali hiyo.
Mabadiliko ya tabiachi yameziathiri kwa kiasi kikubwa sekta za kilimo na usafiri wa majini ambapo uzalishaji wa mazao umeshuka kutokana na uhaba wa mvua na pia kuyeyuka kwa barafu kulikosababishwa na ongezeko la joto kwenye eneo la Antarctic.
Akizungumzia athari kwa upande wa hifadhi za Taifa, Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi Tembo, Dk Alfread Kikoti ametoa tahadhari kwamba iwapo hazitachukuliwa hatua za makusudi kukabiliana na hali hiyo kuna hatari ya Tanzania kubakiwa na hifadhi mbili ifikapo mwaka 2050 kati ya 16 zilizopo.
Mkurugenzi huyo alizitaja hifadhi hizo ambazo utafiti unaonyesha zitabakia kuwa ni Ruaha na Selou kutokana na sababu ya hali ya kijiografia pamoja na ikolojia. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo mabadiliko ya tabianchi yataleta athari kwenye hifadhi zingine ikiwamo ukame utakaotokana na kukauka kwa maji na malisho ya wanyamapori.
Alisema ili kunusuru kupotea kwa hifadhi hizo, inahitajika mikakati madhubuti itakayohusisha pande zote pamoja na wananchi.
Dk Kikoti alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari uliofunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye aliwaomba kuweka mbele uzalendo wakati wa kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Alain Kijazi alisema vyombo vya habari vimechangia kutangaza vivutio na hivyo kuwavuta wageni kutoka nchi za nje ili kuvitembelea.
Alisema Tanapa itaendelea kuvitumia vyombo vya habari kuielimisha jamii hata katika suala la mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia mambo mbalimbali ikiwamo uhifadhi.
Wahariri waliohudhuria mkutano huo walionyesha hofu juu ya taarifa ya hatari ya kutoweka kwa hifadhi hizo na kuahidi kutumia nafasi zao kuielimisha jamii iweze kukabiliana na mabadiliko hayo.







No comments:
Post a Comment