Mameya wawili wa Chadema wamepanga kumwangukia Rais John Magufuli wakitaka aingilie kati michakato ya maendeleo katika maeneo yao ili ikamilike mapema.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya ametumwa na baraza la madiwani la manispaa hiyo kwenda kuonana na Rais Magufuli ili mchakato wa kuufanya mji wa Moshi kuwa jiji ukamilike.
Naye Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amemuomba Rais Magufuli kuingilia kati mchakato wa Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kwa madai kuwa baadhi ya viongozi wanakwamisha utekelezaji wake.
Kuhusu Moshi kuwa jiji, mchakato huo uliokuwa hatua za mwisho ulisitishwa Aprili 30 mwaka huu na Rais Magufuli alipokutana na viongozi wa dini Ikulu mjini Moshi baada ya mchungaji mmoja kudai Manispaa ya Moshi inataka kuwapora ardhi yao.
Kauli ya Rais Magufuli ilisisitiza kuwa mchakato wa kuifanya Moshi kuwa jiji haukufuata taratibu, lakini tayari Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alikuwa amesaini sheria ya kuviingiza vitongoji 40 katika Manispaa ya Moshi.
Moja kati ya vikwazo vilivyofanya mji huo usiwe jiji ni udogo wa eneo la kilomita za mraba 58, hivyo kulazimisha mazungumzo na halmashauri za wilaya ya Hai na Moshi ili vitongoji hivyo viingie katika Mji wa Moshi.
Kuingizwa kwa vitongoji hivyo 40 kulifanya mji huo kuwa na eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 142 ambao Lukuvi kupitia tangazo la Serikali (GN) namba 219 la Julai 15 mwaka huu, aliviingiza vitongoji hivyo Moshi Mjini.
Suala hilo la kusitishwa kwa mchakato huo, liliibua mjadala mkali wiki iliyopita katika Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi na kufikia azimio la kumtuma meya huyo kwenda kuonana na Rais Magufuli.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mboya alisema tayari alikuwa amefika jijini Dar es Salaam tangu juzi na jana alikuwa na miadi ya kuonana na Waziri Lukuvi ili kuzungumza naye awasaidie kwenda kuzungumza na Rais ili atengue zuio lake.
“Zuio la Rais limekuja wakati tayari tulikuwa tumesaini mkataba wa zaidi ya Sh700 milioni na kampuni ambayo ingeandaa master plan (mpango wa jiji) ya miaka 20 na walikuwa wapo site (eneo la mradi),” alisema Mboya.
“Leo tumesitisha hadi hapo tutakapopata GN kwa vile ile GN ya kilometa za mraba 58 ilifutwa na GN namba 219. Mimi nimuombe Rais apitie mchakato wote ulivyokwenda na ikimpendeza aturudishie ile GN ya kilomita 142,”alisisitiza.
Mboya alisema endapo Waziri Lukuvi atashindwa kumsaidia ili aonane na Rais, atalazimika kufuata taratibu zote za kiitifaki ili aweze kuonana na Rais Magufuli, kumuomba atengue agizo lake la kusitisha mchakato huo.
Meya huyo alisema haamini kama Rais atakubali fedha za walipa kodi zipotee bure kwa sababu mchakato huo ulioanza mwaka 2012 ulihusisha vikao mbalimbali ambavyo viligharimu zaidi ya Sh150 milioni hadi ulipofikia.
Mwaka 2012, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alifanya ziara katika Manispaa ya Moshi na kutaka vikwazo vyote vya kutaka Moshi kuwa jiji vimalizwe ili mji huo uwe jiji ifikapo 2015 kabla hajaondoka madarakani.
Wakati Mboya akifanya hivyo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amemuomba Rais Magufuli kuingilia kati mchakato wa Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kwa madai kuwa baadhi ya viongozi wa chini yake wanakwamisha utekelezaji wake.
Mradi wa DMDP una thamani ya Sh600 bilioni na unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwa lengo la kuboresha miundombinu mbalimbali zikiwamo barabara, mifereji mikubwa sanjari na kudhibiti mafuriko katika halmashauri za Dar es Salaam.
Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema), alitoa ombi hilo jana wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo kilichokuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo kupitia taarifa za utendaji za halmashauri hiyo.
Alisema ni wakati mwafaka wa Rais Magufuli kuingilia kati ili kubaini kinachokwamisha mradi huo usitekelezwe licha ya baadhi ya taratibu kukamilika.
“Ubungo ndiyo waathirika wakubwa wa mradi huu. Katika kipindi cha wiki nimejaribu kuwasiliana na WB na wamenieleza mkwamo walioupata katika utekelezaji, ndiyo maana leo natoa rai kwa Serikali Kuu kuingilia kati,” alisema Jacob.
Alifafanua kwamba WB wamekaa na fedha hizo tangu mwaka 2015/16 na wakati Kinondoni haijagawanyishwa Baraza la Madiwani lilikaa na kukubaliana kukopa fedha benki Sh14 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi watakaopisha mradi huo.
Alieleza kuwa baada ya mgawanyo wa manispaa, Ubungo ilitengewa Sh51 bilioni za DMDP kwa ajili ya kuboresha miradi tisa ikiwamo barabara za Sinza Kijiweni –Mtogole hadi Morocco, Korogwe –Kilungule na Mawasiliano2000 ambazo zimeathirika kutokana mkwamo huo.
Hata hivyo, Mratibu wa DMDP kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mhandisi Emmanuel Ndyamukama alisema hakuna dalili zozote za mradi huo kukwama na kwamba utekelezaji wake unaendelea kwa kasi.
“Serikali ipo imara katika mchakato huu na unakwenda vizuri. Nakushauri tembelea Kinondoni, Ilala na Temeke uone matokeo ya mradi huu, labda meya hajafuatilia kwa umakini, lakini kazi kubwa inafanyika,” alisema Ndyamukama.
Mhandisi Ndyamukama alisema hivi sasa wapo katika mchakato wa kuwatambua na kuwalipa fidia wananchi wakiwamo wa wilaya ya Ubungo ambao watapisha mradi huo na kwamba fedha hizo zipo tayari.
“Agosti katikati tunatarajia kuanza ngwe nyingine ya mradi huu. Nawaomba niwahakikishie mradi upo imara haujasimama na uthibitisho upo katika baadhi ya maeneo unakotekelezwa,” alisema Ndyamukama.
No comments:
Post a Comment