Sungo blog
Spika wa Bunge, Job Ndugai ameliamsha ‘dude’ kuhusu matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu baada ya kueleza kuwa gharama za kumsafirisha hadi Nairobi, Kenya zimetolewa na mbunge wa CCM jambo ambalo limekanushwa na Chadema.
Sakata hilo kama vile lilianzishwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyenukuliwa kwenye mitandao ya kijamii akilalamika kwamba Serikali haikutoa msaada katika matibabu ya Lissu.
Kauli hiyo ya Lema, jana ilimuibua Spika Ndugai ambaye ni kama aliamua ‘kumwaga mboga’ kama wasemavyo vijana wa mjini na kusema Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky ndiye aliyejitolea kufanya utaratibu kwa gharama zake kuagiza ndege kutoka Nairobi kumchukua kwa ahadi ya kurejeshewa fedha zake baadaye.
“Mbunge wa CCM Turky akaagiza hiyo ndege kwa dola 9,200. Serikali hii anayoituhumu huyu Lema ikaruhusu air space ya Tanzania ili ndege iweze kutua. Tukaomba vibali vyote kuhakikisha ndege hiyo inatua hapa Dodoma usiku kinyume na taratibu za Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
“Mgonjwa akapelekwa Nairobi unamlaumu nini Spika? Hivi mimi ndiyo mshahara wa kunipa kweli! Ndugu zangu mkoje? Nyinyi ni watu mkoje? Wagonjwa wangapi wa Bunge wameugua mliwahi kumchangia mgonjwa yupi?” alihoji.
Pamoja na hayo alisema aliwashawishi wabunge kuchangia matibabu ya Lissu kwa kukata nusu ya posho zao na kupatikana Sh43 milioni licha ya wengine kukataa.
Aliwataka wabunge wa upinzani kuwa na utaratibu wa kurekebishana badala ya kubebana mbunge mwenzao anapomtuhumu Spika.
Alisema muda wowote watakapoambiwa kwamba Lissu anapelekwa India, watachukua gharama kwa sababu ndiyo utaratibu wao.
Muda mfupi baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambaye yuko Nairobi na Lissu alijibu mapigo, “Spika Ndugai, muogope Mungu usilete utani katika maisha ya Mh Lissu, umeliongopea Bunge na umma. Gharama zote zimelipwa na Chadema na Watanzania. The Parliament deserve better than you,” aliandika kwenye mitandao ya kijamii huku akiambatanisha ankara ikionyesha kwamba gharama hizo Dola za Marekani 9,000 (Sh19,575,000) zimelipwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Baadaye Msigwa alituma video ikimkariri katika mitandao akisema, “Pamoja na kwamba tupo katika kumuuguza Tundu Lissu, tunalazimika kuweka sawa mambo ya msingi.
“Nianze kwa kusema mimi nakuheshimu, kama kamishna wa Bunge, lakini kwa mwenendo uliokuwa ukienda nao namna ulivyoliongoza Bunge na hasa kulihusisha na jinsi Serikali ilivyokuteka, imekumeza, unashindwa kuliongoza Bunge...”
Msigwa alisema analazimika kuyasema hayo pamoja na kwamba anajua madhara yake. Alidai huo ni uongo na kwamba gharama za ndege hiyo zililipwa na Chadema.
Hata hivyo, baadaye jana jioni Ofisi ya Bunge ilitoa ufafanuzi kuhusu madai ya Spika kulidanganya Bunge ikieleza kuwa ndege hiyo ilidhaminiwa na Turky na kwamba Chadema ililipa fedha hizo jana baada ya kauli ya Spika.”
Katika madai yake, Msigwa alisema anasema hayo kwa ujasiri mkubwa kwa sababu sasa hakuna tena cha kuogopa, akidai kwamba wanazo taarifa za wabunge wanaofuata kudhuriwa kama ilivyotokea kwa Lissu.
“Tunajua anayefuata ni mheshimiwa Mbowe, mimi mwenyewe wiki mbili zilizopita nilifuatwa na vijana nikiwa mkoani Iringa, (Godbless) Lema lakini pia Halima (Mdee) wote tupo katika orodha ya kupigwa risasi sasa tuogope nini tena?” alidai Msigwa.
Alimkumbusha Spika Ndugai wakati wa mauaji ya Kibiti wakati wabunge Lema, John Mnyika na yeye (Msigwa) waliposimama ndani ya Bunge na kutaka lisimame ili kujadili masuala hayo, lakini hakuwasikiliza.
Alisema yuko tayari kufukuzwa ubunge wake, lakini kamwe hatanyamaza kwa sababu Spika huyo ameshindwa kulisimamia Bunge.
“Hatumung’unyi maneno tunajua sasa wabunge wanne tunawindwa, hatuogopi na kwamba lazima mjue roho zetu ziko mikononi mwenu.”
Turky aeleza alichofanya
Akizungumzia utata huo, Turky alisema alichofanya ni kudhamini na si kulipa gharama za ndege hiyo.
Turky alisema anapenda kuiweka Tanzania katika hali ya usalama na ukweli, “Tusifanye tukio la Tundu Lissu kuwa la siasa. Mimi binafsi tukio zima la mbunge mwenzangu limenisikitisha sana limenisononesha sana. Nikiwa kama kamishna wa Bunge lakini pia ni binadamu kuna kuzaliwa na kufa.”
“Kwa hiyo tukio hilo lilipotokea tuliitwa makamishna wote na Spika wetu wakiwemo Mbowe (Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani) Msigwa na timu yake. Kwanza ndege ilikuwepo pale airport ambayo ilikuwa imeshaagizwa na Bunge iko standby kumpeleka moja kwa moja Muhimbili.”
Alisema walichoamua ni kuwa aende moja kwa moja Nairobi lakini ndege hiyo haikuwa na kibali cha kwenda Kenya na kwamba ilihitaji kuwa na marubani wawili.
Alisema Spika Ndugai alihangaika kupata kibali cha ndege hiyo ili iweze kumpeleka, “Wakati mambo yote tayari rubani wa ndege akasema kuna kitu kinaitwa landing Instrument ambayo ile ndege haina kwa hiyo haitaweza kuruka.”
Alisema kutokana na majibu hayo, waliingiwa na sitofahamu ndipo alipotafuta ndege kwa ndugu zake ambao anafanya nao biashara.
“Nikawaambia ndege ipo wakatoa nauli zao za ghalighali kwa sababu tunajuana wakakubali kutusaidia kwa dola 9,200 pamoja na ambulance (gari la wagonjwa) mimi ndiyo niliyoita kwa kukubaliana na Mbowe na Msigwa kwamba Turky haya mambo yasimamie baadaye…na ndicho kilichofanyika.”
Alisema walitakiwa walipe siku ya pili lakini haikuwezekana. Alisema kama Chadema isingelipa fedha hizo hadi jana, ingebidi atoe za kwake kulipa deni hilo, “Kwa sababu wale mabwana watakuwa wamepitiliza bahati leo (jana) mchana nimempigia mwenye ndege saa 6.30 mchana ndiyo akaniambia kuwa wamelipa.”
Ndugai na mijadala mitandaoni
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Ndugai ametumia sehemu ya muda wake kuwajibu wabunge watatu wa upinzani ambao amedai wamekuwa wakimtuhumu na kulidhalilisha Bunge kupitia mitandao ya jamii nchini.
Wabunge hao, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Saed Kubenea (Ubungo) wote wa Chadema) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini- ACT –Wazalendo), wamekuwa wakimshutumu Spika kwa mambo mbalimbali katika mtandao.
Akizungumza bungeni jana baada ya matangazo ya wageni, Ndugai alisema kwa wabunge ambao walikuwa wakifuatilia vyombo vya habari wameona katika mitandao ya kijamii Lema akimshambulia.
“Na nitajitahidi kuongea kwa upole sana. Kwanza amemshutumu Spika kwa nini Kubenea ameitwa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama nahisi kuwa ni mmoja wa wabunge ambaye hayupo pamoja nasi, sipendi kumuita mtoro lakini hajakuwepo pamoja nasi baadhi ya mambo yamempita kidogo,” alisema Ndugai.
Alisema wabunge waliamua bungeni kuwa mambo yanayohusiana na usalama yapelekwe katika kamati hiyo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kutoa mawazo hayo.
“Kwa hiyo mambo haya yameenda huko, hayo aliyoyasema Kubenea yanaweza kuisaidia kamati katika kufanya kazi yake kwa hiyo hapelekwi kama mtuhumiwa wa jambo lolote, anapelekwa ili hayo anayoyasema huko mabarabarani, badala ya kuyasema mabarabarani huko kama mbunge akayaseme kwa wenzake ili kamati hiyo itakapoleta ripoti yake hapa kama mlivyoiomba, hayo nayo yawe sehemu ya ripoti hiyo, sasa anachozoza huko Nairobi ni kitu gani? Hata wewe (Lema) uliyonayo tuna kamati hapa. Lete hayo mambo yako iwe kwa WhatsApp, iwe kwa Facebook, kwa Twitter iwe kwa utaratibu gani wowote ule hata mwenyewe uje physical.”
Ndugai alisema upotoshaji huo si jambo jema na kuomba yeyote mwenye habari zozote kuhusu mambo yote ya Lissu, ayapeleke katika ambayo alisema ipo na inafuatilia badala ya kupotosha wananchi.
“Kwanza niseme si vyema sana tunapokuwa na mbunge mwenzetu Lissu katika hali aliyokuwa nayo na mwingine anatake advantage ya kuanza kushutumu wengine na kujiweka yeye kama ndiyo mpendwa sana ila wengine kama mashetani fulani si vizuri na kwa mtu mstaarabu hufanyi hivyo.”
Matibabu kwa wabunge
Spika Ndugai pia alizungumzia madai ya kwamba Serikali imekataa kumtibu mbunge huyo, “Katika mjadala tuliokuwepo nao sisi kwa pamoja kuhusu taratibu zetu na nyinyi mnazijua,” alisema na kuongeza:
“Sisi wote tuna bima pamoja na mawaziri hapa, na bima yetu inafanana na ni National Health Insurance Fund (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya- NHIF) bima yetu tunatibiwa katika hospitali hii yetu ya mkoa au hospitali nyingine za Serikali, rufaa yetu ni Muhimbili, baada ya hapo ni kupelekwa India katika Hospitali za Apollo.”
Alisema Lema amemtuhumu kuwa yeye (Spika) alikwenda kutibiwa kwa gharama kubwa na kwamba habari ya gharama yeye hawezi kufahamu kwa sababu anatibiwa kwa kutumia bima ya afya.
“Suala la gharama si tatizo kama nilikuwa nimeenda huko kucheza disko ungeweza kunilaumu lakini nilienda kama mgonjwa kwelikweli. Na kwa mwaka huu katika haya matibabu sikuwa pekee yangu humu ndani, lakini (James) Mbatia (Mbunge wa Vunjo-NCCR- Mageuzi) yuko hapa na wewe umetibiwa India,” alisema na kuendelea:
“Hiyo ndiyo bima yetu wote, kama mimi ningetibiwa Nairobi ndiyo mngenilaumu. Suala la Nairobi tulikaa na Mbowe alisema wao na familia wanahisi mgonjwa akatibiwe Nairobi.”
Alisema Mbowe anawaamini madaktari wa Tanzania, kwa uwezo wao na weledi wao na vifaa vyao, lakini aliomba mgonjwa kupelekwa Nairobi kwa sababu familia hiyo itakuwa na amani zaidi.
Alisema walikuwa makamishna wengi wa Tume ya Utumishi ya Bunge akiwamo Mbowe na ulielezwa utaratibu na kiongozi huyo wa Chadema alisema chama chake kitabeba gharama hizo.
“Haya yote yanazungumzwa ndege ya NHIF ilikuwa inamsubiri uwanjani, wabunge mmewahi kuugua ni yupi alikuwa anaugua ama kufa ambaye ndege ilikuwa uwanjani inamsubiri? Na ndege ilikuwa standby (tayari) tangu tukio lilipotokea hadi saa 6.00 usiku,” alisema.
“Ni mazito kusema. Kwa jinsi ninavyosononeshwa na ninavyoendelea kusononeshwa, kwa kweli namsamehe huyu mtu (Lema) hajui atendalo na wote tumsamehe tu. Kwa watu wa Arusha niwaambie jambo moja tu Arusha deserve better,” alisema akimaanisha Arusha inastahili kitu bora.
Mbowe azungumzia hali ya Lissu
Wakati hayo yakiendelea hali ya Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi Alhamisi iliyopita akiwa nje ya nyumba yake mjini Dodoma mchana imeimarika na mpaka jana mbunge huyo alikuwa anaweza kuongea na kula kidogo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Nairobi, Mbowe alisema taarifa za kwamba Lissu amepata maambukizo katika kifua ambayo yanatishia maisha yake siyo za ukweli.
Alisema afya yake inaimarika kila siku na kuwahakikishia wananchi kuwa anaendelea kurejea katika hali yake. Alisema mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, alionana na baadhi ya watu waliomtembelea.
“Pamoja na kwamba kuna watu wengi wanataka kumuona lakini ni wachache wanaoruhusiwa kwa kuwa madaktari (hospitali ya Nairobi) wanataka apumzike,” alisema.
No comments:
Post a Comment