Watu sita wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi katika mtaa wa Fumagila Mashariki Kata ya Igoma jijini Mwanza.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo baada ya watu hao kuzingirwa katikati ya majengo mtaani hapo na kufanya mashambulizi ya kujibizana risasi kwa muda mrefu.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akaomba alitolee ufafanuzi baadaye kwa kuwa hivi sasa bado anaendelea kukusanya taarifa zaidi.
“Ni kweli hilo tukio hilo lipo, ila bado tunashughulikia naomba munipe muda nitataoa ufafanuzi baadaye,” alisema kwa ufupi Kamanda Msangi.
Shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni diwani wa Kata ya Kishili iliyo jirani na kata hiyo, Sospeter Ndumi amesema kurushiana risasi baina ya watu hao na polisi kulianza usiku wa manane hadi majira ya asubuhi.
Amesema katika majibizano hayo polisi walifanikiwa kuwaua watu hao na kukamata silaha mbalimbali za kivita walizokuwa wanazitumia.
Katika mtaa huo huo ndipo lilipotokea tukio la Desemba 3 mwaka jana ambapo polisi waliwakamata watoto 11 wenye umri unaokadiriwa kuwa na miaka sita hadi 14 baada ya kuizingira nyumba moja kwa lengo la kuwakamata watu waliowahisi kuwa majambazi.
Mmoja kati ya watu watatu waliokutwa kwenye nyumba hiyo alikimbia baada ya kuwarushia polisi bumu la mkono, kabla ya polisi kuwadhibiti waliosalia kwa kushirikiana na wananchi wa mtaa huo.
Kadhalika katika tukio hilo, watu watatu waliosadikiwa kuwa ni majambazi waliuawa na bunduki mbili aina ya SMG na AK47, magazine saba, bastola moja na risasi 183 vilikamatwa na polisi.
Baada ya polisi kuondoka katika eneo hilo, wananchi waliiteketeza nyumba hiyo kwa moto.
No comments:
Post a Comment