Breaking




Friday, 25 August 2017

TFF yaomba radhi , yakubali kukosea Shield Cup


Faridi Miraji , Dar es salaam.                           

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewaomba radhi wanafamilia wote wa mpira wa miguu nchini kutokana na makosa ya maandishi yaliyoonekana kwenye utambulisho wa Ngao ya Jamii iliyotolewa Jumatano Agosti 23, 2017.

Ngao hiyo ilitolewa mara baada ya mchezo uliokutanisha timu za Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini. Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Yanga na kutwaa Ngao hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa jana, watumiaji mbalimbali wa mitandao ya kijamii walikosoa kitendo cha ngao hiyo ya jamii kukosewa maandishi ambayo yalisomeka Community Sheild badala ya Community Shield .

Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho hilo mapema leo ilisomeka hivi, “Watanzania hususani wanafamilia wa mpira wa miguu popote pale, TFF hatujapokea vizuri mwonekano wenye makosa kwenye Ngao hiyo ya Jamii kama ambavyo wadau hawajapokea vema suala hili”

Hata hivyo taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa adhabu kali itatolewa kwa wale wote ambao walihusika kwenye utengenezaji huku wakiitaka klabu ya Simba kurudisha ngao hiyo kwa ajili ya kuifanyia marekebisho.

“Kutokana na makosa hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, tayari amechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika kadhalika kuwasiliana na uongozi wa Simba SC kuirejesha Ngao hiyo ili kufanyiwa marekebisho yatakayobaki kwenye kumbukumbu sahihi. Hatutegemei tukio kama hili kujirudia tena”, ilieleza taarifa hiyo

No comments:

Post a Comment