Sungo blog
MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Igunga, mkoani Tabora, Ramadhani Hassan (15), mkazi wa Mtaa wa Nkokoto, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo alipokuwa akichota maji kwenye mashimo ya mto Mbutu.
Diwani wa Kata ya Igunga Mjini, Charles Bomani, alisema mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani kwao Oktoba Mosi, mwaka huu asubuhi kwa kutumia baiskeli akiwa na amebeba ndoo tupu kwa ajili ya kufuata maji ya kutumia katika mto Mbutu, kutokana na tatizo sugu la uhaba wa maji wilayani Igunga.
Diwani Bomani alisema hakurejea nyumbani kwamba na kesho yake wazazi wake walitoa taarifa katika kituo cha Polisi Igunga na jitihada za kumtafuta mwanafunzi huyo zilifanyika na Ijumaa asubuhi ndipo mwili wa kijana huyo ulikutwa katika mto Mbutu ukiwa umekandamizwa na kifusi cha udongo.
Kwa mujibu wa Diwani Bomani, pamoja na kuupata mwili huo, pia waliikuta baiskeli na ndoo vikiwa eneo hilo.
Bomani aliwataka wazazi kuwafuatilia watoto wao wanapokwenda kutafuta maji katika mto Mbutu kwa kuwa ardhi hiyo ina mpasuko, hali ambayo ni hatari kwa wanaochimba visima kwenye mto huo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, Buswelu Ikieleiya, alieleza kusikitishwa na alisema kifo cha mwanafunzi huyo na kuwa asilaumiwe mtu kwa kuwa ni mipango ya Mungu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Melchades Magongo, alithibitisha kupokea maiti ya mwanafunzi huyo na kuongeza kuwa wameshawakabidhi ndugu na tayari mwili huo ambao ulizikwa katika makaburi ya Masanga.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi, Willibrod Mutafungwa, alisema hajapokea taarifa yeyote juu ya kifo cha mwanafunzi huyo.
“Mimi sijapokea taarifa ya kifo cha mwanafunzi, lakini OCD Igunga anafuatilia tukio hilo,” alisema Mutafungwa.
No comments:
Post a Comment