Sungo blog
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Andrea Kigwangalla ambaye jana ameteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii amefunguka na kushukuru kwa kuaminiwa.
Kigwangalla amesema jana alipata taarifa ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii akiwa katika ziara ya Kituo cha Afya Kilimarondo Wilaya ya Nachingwea hivyo ilibidi safari yake kuisha na kuanza kutoa namba za gari lake kama Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
"Baada ya kupata taarifa hiyo kila kitu ilibidi kisimame hapo hapo. Namba za NWAMJW ilibidi ziondolewe na safari ya kutoka huko ianze! Nimepokea salamu nyingi za pongezi na shukrani kwa Mungu aliye juu. Sintoweza kumjibu kila mtu, uungwana ni kutambua pongezi zenu na dua tele mlizotuombea, nawashukuru sana ndugu zangu. Tuzidi kuombeana dua tu" alisema Kigwangalla
Aidha Waziri huyo wa Maliasili na Utalii alisema kuwa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kukidhi matarajio ya Rais John Pombe Magufuli ambaye amemuamini na kumpa nafasi ya juu zaidi katika serikali ya awamu ya tano.
"Tuna kazi ngumu ya kukimbia kukidhi matarajio ya kiongozi wetu mkuu aliyetuamini, na matarajio ya wananchi wenzetu. Binafsi nawaahidi nyote kuwa sintowaangusha!Ahsanteni sana ndugu zangu, natarajia ushirikiano wenu wa kila hali" alisema Kigwangalla
No comments:
Post a Comment