Breaking




Friday 6 October 2017

KIMBUNGA NATE CHAWAUA WATU 20 AMERIKA YA KATI


Sungo blog

Kimbunga Nate kimewaua watu zaidi ya 20 nchini Costa Rica, Nicaragua na Honduras huku kikielekea kaskazini upande wa Marekani.

Hali ya dharura imetangazwa katika mataifa kadha ya Amerika ya Kati ambapo watu zaidi ya 20 bado hawajulikani walipo.

Kimbunga hicho kimesababisha mvua kubwa, maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Barabara nyingi hazipitiki, madaraja yameporomoka na pia kimesababisha uharibifu mkubwa kwenye nyumba za watu na majengo.

Nchini Costa Rica, watu karibu 400,000 hawana maji na maelfu wengine wameachwa bila makao na wanalala kwenye vyumba vya muda.

Watu zaidi ya sita wamethibitishwa kufariki katika taifa hilo, Watu wengine 11 waliuawa kimbunga hicho kilipokuwa kinaelekea kaskazini na kufika Nicaragua, Watu watatu wameuawa nchini Honduras na kuna watu kadha ambao hawajulikani waliko.

Nchini Costa Rica, safari zote za treni zimesitishwa na safari kadha za ndege pia zimefutwa.
Mbuga kadha za taifa ambazo ni maarufu kwa watalii pia zimefungwa kama tahadhari, Kimbunga hicho pia kimesababisha uharibifu mkubwa kwenye miundo mbinu Nicaragua.

Watabiri wanasema kimbunga Nate kitaimarika na kuwa kimbunga cha ngazi 1 kabla ya kufika tena ardhini pwani ya kusini mwa Marekani siku ya Jumapili.

Kampuni za mafuta zinazohudumu katika Ghuba ya Mexico zimesema zinawahamisha watu kutoka kwenye visima vyake ambavyo vipo maeneo ambayo inatarajiwa kimbunga hicho kitapitia.




No comments:

Post a Comment