Sungo blog
Emmanuel Okwi ameendelea kuwa shujaa wa Simba baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa timu hiyo katika dakika ya 94 kwenye kipute dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Simba imepata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa katika mtanange huo uliopigwa kwenye Dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara jioni ya leo.
Matokeo hayo yanaifanya Simba na Mtibwa Sugar zote zifikishe pointi 12 baada ya kucheza mechi sita, sawa na Azam FC na Yanga, za Dar es Salaam pia.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shakaile Shangalai kutoka Pwani, aliyesaidiwa na Janet Balama wa Iringa na Sylvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Stahmili Mbonde dakika ya 35 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na beki wa zamani wa Simba, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
Kipindi cha pili, Kocha Joseph Omog alikianza kwa kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi, akimtoa beki Salim Mbonde aliyeumia na kumuingiza Mganda, Juuko Murshid.
Mtibwa Sugar ilipata pigo dakika ya 57, baada ya Mbonde kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake akaingia Kelvin Sabato Kongwe.
Dakika ya 90 na ushei, beki Cassian Ponera akamvuta beki wa Simba nje kidogo ya boksi na refa Shakaile Shangalai akatenga mpira wa adhabu ambao Okwi alikwenda kupiga kiufundi na kuisawazishia Simba.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni, Salim Mbonde/Juuko Murshid dk46, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Said Ndemla dk63, James Kotei, John Bocco, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
Mtibwa Sugar; Benedict Tinoco, Salum Kanoni, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daud, Cassian Ponera, Shaaban Nditi, Salum Kihimbwa/Henry Joseph dk89, Mohamed Issa, Stahmil Mbonde/Kevin Sabato dk57, Salum Khamis/Hassan Dilunga dk69 na Ally Makarani.






No comments:
Post a Comment