Saturday, 23 December 2017

URASIMU WAIONDOA KAMPUNI YA UMEME KENYA , YAJIPANGA KUHAMIA TANZANIA

Sungo blog

Kampuni ya nchini Sweden iliyotaka kujenga mtambo mkubwa zaidi Afrika Mashariki wa kufua umeme kwa kutumia upepo huko Malindi, Kenya,  kwa gharama ya shilingi za kitanzania 253 billioni, imehamishia uwekezaji huo nchini Tanzania, kufuatia kutokuwepo kwa maelewano mazuri na serikali ya Kenya.

Mwaka jana kampuni ya VR Holding AB ilieleza lengo lake la kujenga mitambo ya kufua umeme kwa kutumia upepo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 600, katika rasi ya Ngomeni mjini Malindi, lakini Wizara ya Nishati nchini Kenya ikalikataa mbi lao kwa madai ya kutokuwepo kwa mfumo wa miradi ya nishati mbadala ya kiwango hicho pamoja na uhitaji wa umeme kuwa mdogo nchini hapo.

Wakurugenzi wa kampuni hiyo wameeleza kuwa, kwa sasa wamebadili mtazamo wao na kuiangalia zaidi nchi ya Tanzania ambayo pia iko katika ukanda huo huo wa Bahari ya Hindi.

“Tumeamua kutafuta ufumbuzi kwa ajili ya Tanzania” alisema Victoria Rikede, Mkurugenzi katika kampuni hiyo.

“Kenya imeonekana kuwa na ugumu kiasi na pia haitoweza kutumia kiasi chote cha umeme utakaozalishwa katika gridi hiyo. Hivyo kwa sasa ufumbuzi kwao ni kujenga gridi ndogo,” aliongeza.

Nchi ya Kenya inayoongoza kwa kuwa na uchumi mkubwa Afrika Mashariki imeonakana kupoteza baadhi ya fursa kubwa za uwekezaji kama vile bomba la mafuta ambalo limehamishiwa Tanzania.

Wizara ya Nishati nchini humo ilieleza kuwa kujengwa kwa mtambo huo mkubwa wa kuzalisha umeme, kungeifanya nchi hiyo kuwa na umeme mwingi kuliko mahitaji na hivyo  kuwafanya wananchi wake kulipa gharama kubwa za umeme ambao hautotumika.

Taarifa zinaeleza kuwa nchi ya Kenya iliitaka Kampuni hiyo kujenga mtambo mdogo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 50.

No comments:

Post a Comment