Sungo blog
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amepokea vituo sita vya polisi vinavyohamishika kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, huku akibainisha kuwa eneo hilo lina matukio mengi ya uhalifu.
Vituo hivyo vilivyotolewa na kampuni ya vinywaji baridi ya CocaCola vimekabidhiwa leo Alhamisi Machi15, 2018.
Akipokea vituo hivyo, Masauni aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo uliolenga kuimarisha ulinzi na usalama na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo.
Amesema wameamua vituo hivyo kuwepo Kinondoni kutokana utafiti uliofanyika unaoonyesha mkoa huo wa kipolisi kuongoza kwa matukio ya kihalifu kwa Jiji la Dar es Salaam.
"Mipango yetu ya baadaye vituo kama hivi viwepo Dodoma makuu ya mji ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuwa mjini kunakuwa na Serikali imeshahamia huko," amesema Masauni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo amesema vituo hivyo vitawekwa katika maeneo ambayo hayana huduma za kipolisi na yenye changamoto za kihalifu.
"Vituo hivi ni vya kisasa na vimeboresha zaidi kwa kuweka huduma za msingi ikiwemo maliwato tofauti kidogo na vile vya awali. Tutahakikisha vinatumika ipasavyo ili kuwasaidia wananchi," amesema Kamanda Murilo.
No comments:
Post a Comment