Breaking




Saturday, 29 July 2017

UTATA WAIBUKA WAVUVI WATATU WALIOPIGWA RISASI DAR





Wavuvi watatu wanadaiwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana huku mmoja akidaiwa kupoteza maisha katika eneo la Minazi Mikinda lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea Julai 25 saa nane mchana, ambapo wavuvi hao walikuwa katika eneo hilo la ufukwe wa Bahari ya Hindi baada ya kutoka kuvua samaki.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana, wavuvi hao wanadaiwa kukutwa na tukio hilo walipofuatwa na watu waliowataka kuonyesha leseni zao uvuvi. Chanzo cha habari hii kilisema baada ya kufuatwa na watu hao, pia walianza kushurutishwa kwa kuamriwa kulala chali.

Inaelezwa kwamba licha ya kutii amri walipigwa risasi huku mmoja akipoteza maisha na wenzake kujeruhiwa na kwamba, wako katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako wanapatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari hii wavuvi waliopigwa risasi wametajwa kwa majina ya Kassim Juma, Ally Madaba na Juma Masoud (ambaye ni marehemu).

Mwenyekiti Msaidizi wa Umoja wa Wavuvi katika eneo hilo, Amir Amani alikiri kutokea kwa tukio hilo. “Haikuwa lazima (kama ni vyombo vya dola) kutumia nguvu waliyoitumia kwani wangeweza kuwakimbiza na kuwakamata iwapo waliwakimbia,” alisema.

Awali, mwenyekiti wa umoja huo, Ally Yusuph alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo simu yake ya kiganjani haikuweza kuita, lakini Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo lina kikosi cha wanamaji kinachoshughulikia pia masuala ya usalama baharini, James Macheta alisema hana taarifa ya tukio hilo.

Macheta alisema atafuatilia kujua undani wa tukio hilo ambalo limeibua hofu kwa wavuvi wanaotumia ufukwe huo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa aliliambia gazeti hili kuwa hana taarifa zozote.

Hata hivyo, Msemaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Almas Jumaa alisema anachofahamu ni kuwa watu hao walipokewa katika Hospitali ya Muhimbili, lakini hawakufikishiwa Moi.

No comments:

Post a Comment