WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua meli mbili za mizigo Mv Njombe na Mv Ruvuma zitakazotumika katika kusafirishia mizigo katika ziwa Nyasa na kuonya kwamba zisitumike kama eneo la kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu sh. Bilioni 11.253 ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli alizozitoa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika ziwa Nyasa.
Amesema ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi, ambapo awali suala hilo lilikuwa likifanywa na raia wa kigeni.
Awali,Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja na kwamba baada ya kukamilisha kazi hiyo, TPA imeingia mkataba na kampuni hiyo ya kizalendo kwa ajili ya ujenzi wa meli ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo kwa gharama ya Sh. bilioni 9.12.







No comments:
Post a Comment