Breaking




Tuesday, 1 August 2017

BENKI NAZO ZIMEANZA KUISOMA NAMBA




Ahueni iliyoanza kujitokeza kwenye sekta ya fedha nchini, imepigwa dafrao baada ya faida ya benki kubwa kupungua kwenye robo ya pili ya mwaka huu.

Itakumbukwa, benki hizo ziliyumba kuanzia robo ya tatu mwaka jana kutokana na mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na Serikali ikiwamo kuhamisha akaunti zote za taasisi za umma kutoka benki za biashara kwenda Benki Kuu (BoT).

Ingawa taasisi hizo zilianza kwa faida, bado ilikuwa chini ya iliyopatikana mwaka jana. Hili linathibitishwa na taarifa za benki za NMB na CRDB ambazo zinaongoza kwa amana na idadi ya wateja, ukubwa wa mtaji na mtandao wa matawi ndani na nje ya nchi.

Kwenye robo ya pili; Aprili mpaka Juni, Benki ya NMB ilipata faida ya Sh35.29 bilioni ikiwa ni chini kulinganisha na ile iliyopatikana kwenye robo ya kwanza au kipindi kama hicho mwaka jana. Kwenye robo iliyoishia Machi, benki hiyo ilipata faida ya Sh40.9 ambayo inafanya faida kuwa nusu mwaka huu, ambayo ni Sh76.2 bilioni ikiwa ni pungufu kwa Sh8.1 bilioni ya iliyopatikana kwenye kipindi kama hicho mwaka jana.

Ndani ya muda huo, NMB imeongeza watumishi 103 kutoka 3,316 waliokuwapo mwaka jana. Ndani ya muda huo pia, imeongeza matawi kutoka 178 mpaka 201. Ingawa ipo chini ya kiwango kinachopendekezwa na kanuni za BoT, uwiano wa mikopo isiyolipika na ile ghafi imeongezeka kutoka asilimia 4.6 mwaka jana, mpaka asilimia 4.9 mwaka huu.

Kwa upande wa Benki ya CRDB yenye thamani ya Sh5.49 trilioni, faida yake baada ya kodi, imepungua kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka Sh27.47 bilioni mwaka jana mpaka Sh13.39 bilioni kwenye robo ya pili. Pamoja na matawi yake yaliyopo Burundi, faida hiyo imepungua pia kutoka Sh28.5 bilioni mpaka Sh13.74 bilioni mwaka huu. Uhakiki wa watumishi hewa pamoja na kusitishwa kwa mishahara ya wenye vyeti feki, kumeendelea kujidhihirisha kwenye taasisi za fedha nchini. Kiwango cha uwiano wa mikopo isiyolipika kwa Benki ya CRDB kimeendelea kuwa juu ya asilimia tano zinazopendekezwa na kanuni za BoT. Ingawa uwiano huo umeshuka kutoka asilimia 14 zilizokuwapo mwaka jana mpaka asilimia 13 mwaka huu, lakini bado upo juu ya unaoshauriwa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omary Mbuta alisema mwenendo huo unamaanisha mambo mengi ya kuzingatiwa ikiwamo ushindani kutoka benki ndogo. “Hali hii inadhihirisha kwamba zilikuwa zinafanya zaidi biashara na Serikali hivyo kujiondoa kwake na mabadiliko mengine yaliyofanywa, kumeziathiri,” alisema Dk Mbura.

Kujiondoa kwa taasisi za serikali kwenye benki hizi, kulipunguza amana za wateja wa benki za biashara kwa zaidi ya Sh900 bilioni huku CRDB pekee ikipoteza zaidi ya Sh700 bilioni. Kutokana na ukweli huo, alizitaka kubadili mikakati ili kuendana na ukweli wa mwenendo wa soko. “Wafanyakazi wanaowaajiri wanatakiwa kuongeza ushindani sokoni hasa kuziona fursa zilizopo kwenye sekta binafsi,” alisema.

Hali ilikuwa tofauti Benki ya NBC ambayo imepata faida ya Sh5.2 bilioni kwenye robo ya pili ikiongezeka kutoka Sh3.39 bilioni iliyopatikana kwenye robo iliyoishia Machi mwaka huu. Ufanisi wa benki hii umetokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo ya riba; kutoka Sh28.8 bilioni za Juni 2016 mpaka Sh33.86 bilioni mwaka huu. NBC, CRDB na NMB ndizo benki zenye idadi na amana kubwa za wateja huku matawi yake yakifika maeneo mengi; NBC inayo 51 hivyo kwa pamoja kuwa na zaidi ya nusu ya matawi yote yaliyopo nchini.

Licha ya benki hizo mbili, hali imekuwa hivyo kwa Exim ambayo faida yake imepungua kwa zaidi ya robo tatu kwa miezi sita ya mwanzo. Benki hiyo imepata faida ya Sh13.95 bilioni kutoka Sh57.85 bilioni zilizopatika mpaka Juni mwaka jana.

Ndani ya miezi mitatu ya robo ya pili, uwiano wa mikopo ghaf isiyolipika imeongezeka kutoka asilimia 9.02 iliyokuwapo robo iliyoishia Machi na kufikia asilimia 12.44. Pia, ukuaji wa amana za wateja unashuka kwa asilimia 1.42 baada ya kuwa asilimia 0.71 kwenye robo ya kwanza.

Kilichofanywa na NBC kilitokea Standard Chartered pia ambayo ilipata faida ya Sh9.9 bilioni mwaka huu kutoka Sh7.8 bilioni zilizokuwapo kipindi kama hicho mwaka jana.




No comments:

Post a Comment