Breaking




Tuesday, 1 August 2017

WAZIRI UMMY MWALIMU AWACHONGEA WAKUU WA MIKOA KWA RAIS MAGUFULI





Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameahidi kumwandikia barua Rais John Magufuli ili aongeze kigezo kipya cha utendaji kazi kwa wakuu wa mikoa nchini.

Waziri huyo alisema anataka idadi ya wananchi waliojiunga na Bima ya Afya kwenye Mkoa na Wilaya iwe moja ya kigezo cha wahusika kuendelea kushika nyadhifa zao.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Kadi ya Matibabu kwa Watoto (Toto Afya Card) inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy alisema Bima ya afya inapaswa kuwa agenda ya kudumu kwenye vikao vya wakuu hao ili kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na kadi ya matibabu.

“Nikitoka hapa nakwenda kuandika barua kwa Rais Magufuli ili aongeze kigezo hiki kwenye vigezo anavyowapima navyo wakuu wa wilaya na mikoa," alisema Waziri Ummy kwa sababu "tunataka wananchi wengi wajiunge na Bima ya Afya na kuwa na uhakika wa kupata matibabu.”

Mwalimu alisema pia atawasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Technoloji, ili kuangalia uwezekano wa kuongeza kiasi cha fedha za matibabu kwenye shule cha Sh. 20,000 kwa kila mwanafunzi na kuwa Sh. 50,400 ili kuwaunganisha na huduma hiyo mpya kwa NHIF.

“Tulianza na vyuo vikuu vyote vinatoa huduma hii, tunakwenda sekondari ambako kwa sasa wanachangia Sh. 20,000 lakini mtoto akiugua anarudishwa nyumbani na mzazi anahangaika na matibabu," alisema.

"Huu ni wizi, tunataka uwepo utaratibu wa kukata Bima.”

Waziri huyo aliuagiza uongozi wa NHIF uwafate wateja kwenye bar, hoteli na sehemu nyingine badala ya kuwasubiri ofisini, huku akieleza kuwa atafuatilia kuona utekelezaji na kutaka sehemu hizo kuwe na uhamasishaji.

“Mkienda maeneo ya bar na sehemu nyingine za starehe mtawapata wateja wengi kwa kuwa unakuta mtu anatumia Sh. 100,000 kunywa pombe na kutoa ofa lakini mwanaye hana kadi ya Bima, kukiwa na wahamasishaji ataandikisha watoto kwa fedha hiyo na familia yake itafaidika kwenye matibabu,” alisisitiza na kusema zaidi:

“Kuna wale waswahili wenzangu wanapenda kutunzana mabeseni ya hadi Sh. 500,000 huku hawana Bima ya Afya, sasa nawashauri wakate Sh. 50,400 wawape Bima watoto wao alafu nyingie akatoe zawadi.”

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kuna Watanzania wanateseka kwa kukosa fedha za kugharamia matibabu na kuwataka wananchi kuwekeza kwenye afya kwa manufaa ya baadaye na kuahidi kuboresha huduma Bima kwenye Hospitali, Vituo vya afya na Zahanati.

Awali, Kaimu Mkurigenzi wa NHIF, Bernard Konga, alisema asilimia 33 ya Watanzania ambao ni wastani wa watu Milioni 16.6 wanatumia huduma za Bima ya Afya, na ifikapo 2020 watafikia asilimia 50 na ikiwa ni sheria rasmi watawafikia asilimia 80.




No comments:

Post a Comment