Breaking




Friday 7 July 2017

KUMBUKUMBU: TRL YAPOKEA VICHWA 2 VYA TRENI KATI YA 13 VILIVYOAGIZWA (MACHI 2015

Vichwa 2 vya treni kati ya 13 vilivyopokelewa bandari ya Dar es Salaam.

Machi 21, 2015 tumeshuhudia tukio muhimu sana kwa TRL kupokea sehemu ya vichwa vipya vya treni vilivyoagizwa kutoka nje ya Nchi. Tumepokea vichwa viwili (2) kati ya vichwa kumi na tatu (13) vya treni vilivyonunuliwa na TRL kupitia bajeti ya Serikali.

Vichwa hivi vimetengenezwa kupitia mkataba kati ya TRL na Kampuni ya EMD ya Marekani. Utengenezaji wa vichwa hivi vya treni umefanyika na Kampuni ya DCD ya Afrika Kusini.

Ununuzi wa vichwa kumi na tatu (13) vya treni umegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 70.9 ambazo zote zimeshalipwa.

Hivi vichwa 13 vipya vinategemewa kupokelewa na TRL katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ni hii tulioshuhudia Machi 21, 2015 ambapo tulipokea vichwa viwili. Awamu ya pili itahusu kupokea vichwa vitano (5) ambavyo vinategemewa kuwasili Mwezi Aprili, 2015. Awamu ya tatu itahusu kupokea vichwa vingine sita ambavyo vinategemewa kuwasili mwezi Juni, 2015.

Vichwa hivi vipya vya treni vimetengenezwa kwa kutumia tekinologia ya kisasa ya kielekroniki zaidi, na vina uwezo zaidi wa kubeba mizigo ikilinganishwa na vichwa vya zamani. Kichwa kimoja kipya kina uwezo wa kusafirisha tani 32,500 kwa mwaka, ukilingalinisha na tani 25,000 kwa mwaka zinazosafirishwa na kichwa cha zamani. Ina maana kwamba kupatikana kwa hivi vichwa vipya kutaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa TRL. Vile vile kuwasili kwa vichwa hivi kutaiwezesha TRL kuendesha treni za abiria mara tatu kwa wiki kutoka mara mbili kwa wiki hivi sasa. Treni ya tatu kwa wiki itaanza safari zake tarehe 1/4/2015.

Mradi huu wa kununua vichwa 13 vipya vya treni ni sehemu tu ya mpango kabambe wa Serikali wa kuifufua na kuiimarisha TRL chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango wa BRN kwa TRL umelenga kuiwezesha Kampuni kiutendaji ili iweze kusafirisha tani milioni 3.0 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016 kutoka tani 200,000 zilizosafirishwa mwaka 2014 kupitia reli ya kati.

Tayari tumeshuhudia hapo nyuma kupokelewa kwa vitendea kazi mbali mbali ambavyo vimeainishwa katika mpango huu.

Vitendea kazi ambavyo tayari vimepokelewa ni pamoja na:

1. Mabehewa 25 ya kubebea kokoto (BHBs)

2. Mabehewa 100 kati ya 274 ya kichele (CLBs)

3. Mabehewa 50 ya kubeba makasha (CCBs)

4. Mabehewa 22 ya abiria

5. Mabehewa 17 kati ya 34 ya breki (BVBs)

6. Mtambo wa kunyanyulia mabehewa (Breakdown crane)

7. Mtambo wa kushindilia kokoto (Tamping Machine)

Kupatikana kwa vitendea kazi hivi pamoja na vingine vitakavyo endelea kupokelewa vitaiwesha TRL kusafirisha mizigo mingi zaidi na abiria wengi zaidi hatimaye kuifanya Kampuni kujiendesha kibiashara na kwa faida na kuacha kuwa tegemezi kwa Serikali.

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL.

Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu

Dar es Salaam,

Machi 23, 2015

No comments:

Post a Comment