Breaking




Monday, 14 August 2017

Ikulu yagoma kulipa mabilioni ya zabuni licha ya Mahakama Kuiamuru Ilipe


Hatimaye Ikulu imesema hailitambui deni la Sh1.6 bilioni ambalo Serikali inadaiwa na kampuni ya GBL and Associates Ltd ya jijini Dar es Salaam baada ya kuinyang’anya zabuni ya kununua na kuuza meno ya tembo iliyoshinda miaka 29 iliyopita.

Uamuzi huo umetolewa licha ya kuwapo hukumu ya Mahakama Kuu inayoeleza wazi kwamba Serikali ilikosea kuifutia kampuni hiyo zabuni iliyoshinda bila sababu za msingi.

Nyaraka zinaonyesha kuwa madai ya GBL yaliwahi kufika mezani kwa marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete ambao waliagiza wasaidizi wao kutafuta ukweli juu ya suala hilo. Tawala hizo zilizopita zilikwishatoa maagizo kampuni hiyo ilipwe.

Mgogoro kati ya Serikali na GBL ulianza mwaka 1988 baada kuinyang’anya zabuni ya kununua tani 16 za meno ya tembo licha kutangazwa mshindi wa mchakato huo na Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Kwa mujibu wa tangazo la zabuni lilitolewa katika gazeti la Serikali la Daily News la Februari 29, 1988 kupitia Bodi ya Taifa ya Zabuni, mshindi wa zabuni hiyo alitakiwa kufanya malipo yote na kukusanya meno hayo ndani ya siku 30 tangu siku ya kukabidhiwa barua ya ushindi.

Hata hivyo, kabla siku hizo 30 hazijatimia, aliyekuwa kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyapori anayetajwa kwa jina la A. Malemaro alimwandikia mmiliki wa kampuni hiyo marehemu Gabriel Lugendo kumjulisha uamuzi wa Serikali kuifutia kampuni yake zabuni kwa kushindwa kulipa fedha ndani ya siku saba, jambo lililozua madai ya muda mrefu.

GBL iliomba zabuni hiyo ikishirikiana na Taathing Ivory Wares ya Hong Kong ambayo ilikwishakopa benki kukamilisha biashara hiyo. Baadaye Serikali ililazimika kurudisha fedha ambazo kampuni hiyo ililipa.

Jaji wa Mahakama Kuu, Yahaya Rubama aliwahi mwaka 1989 kuamua kuwa uamuzi wa kuifutia zabuni hiyo GBL haukuwa wa haki na uvunjwaji wa mkataba.

Awali, kampuni hiyo ilidai Sh507 milioni ambazo ziliongezeka na kufikia Sh4 bilioni pamoja na riba. Hata hivyo, deni hilo lilipunguzwa hadi Sh1.6 bilioni baada ya makubaliano kati ya Serikali na GBL.

Aprili mwaka huu, Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi aliiandikia GBL akiijulisha kuwa Ikulu imepitia malalamiko yake ikiwamo viambatanisho vyake na hitoria ya suala hilo na kuridhika kwamba madai hayo hayana msingi wa sheria.

Balozi Kijazi anasema Ikulu imeridhika kuwa kampuni hiyo ilifutiwa zabuni ya mauzo ya meno ya tembo kwa kushindwa kulipa ndani ya wakati yaani ndani ya siku saba baada ya kupokea barua ya kuarifiwa ushindi wa zabuni.

Kwa mujibu wa barua ya Kijazi ya Aprili 20, kampuni hiyo haikuwa mnunuzi halisi wa meno hayo ila kampuni ya Ms Tathing Ivory Factory ya Hong Kong ambayo hatimaye ililipia meno hayo na fedha hizo baadaye kurejeshwa kwa kampuni hiyo baada ya GBL kufutiwa zabuni.

Anasema ilibainika pia kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyama na Mimea iliyo Hatarini Kutoweka (Cites), kampuni ya Ms Tathing Ivory Factory haikuwa na sifa ya kufanya biashara ya meno ya tembo na nchi zilizosaini mkataba huo, ikiwamo Tanzania.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GBL Thomas Lugendo alisema katika barua yake ya Mei 24 kuwa, Ikulu haijafuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kuwataka kulipa fedha ndani ya siku saba wakati tangazo la zabuni lilitoa siku 30.

“Ikulu inasema tumeshindwa kulipa ndani ya siku saba lakini tangazo la zabuni lilitoa siku 30. Kutuambia tulipe ndani ya siku saba ni kinyume na tangazo la zabuni. Hatukuafiki na hata Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi hakuafiki,” anasema Thomas Lugendo.

Kuhusu madai kuwa kampuni hiyo haikuwa mnunuzi halisi wa meno hayo isipokiwa kampuni ya Taathing Ivory Wares Factory, Lugendo anasema: “Hili ni jambo ambalo isingekuwa vyema kulijibu kwa heshima ya Serikali,” anasema Thomas huku akirejea maneno ya Jaji Rubama.

Jaji Rubama alisema katika hukumu yake: “Katika mwenendo wa biashara za kimataifa, zinazotembea ni karatasi za mikataba. Mimi nimeshinda tenda, nauza kwa mtu mwingine, yule wa mwisho ndiye anabeba mzigo wa fedha ambaye kwa hapa ni kampuni ya Taathing.”

Kuhusu kampuni ya Taathing Ivory Factory kutokuwa katika nchi ambayo ni mwanachama wa Cites, Lugendo alimtaka Balozi Kijazi kurejea tangazo la zabuni lililosema waomba zabuni kutoka nchi wanachama na siyo kampuni zinazonunua.

“Sisi ni Watanzania, maombi yetu yametoka Tanzania kule tutakouzia Serikali haihusiki, hata kama tungechukua meno ya tembo tukayahifadhi kama mapambo yetu. Serikali ilishauza inahusika nini baada ya kuyauza?” alihoji Lugendo.

No comments:

Post a Comment