WAKATI mazungumzo ya Barrick Gold Mine na Serikali yakiendelea juu ya hasara Serikali iliyopata kutokana na udanganyifu wa kampuni hiyo kwenye mchanga wa dhahabu (makinikia), Kamati Maalumu ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mwenendo wa biashara ya tanzanite, inatarajiwa kupeleka kiama kama kilichotokea kwenye dhahabu katika sekta hiyo.
Kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza aina na kiasi cha madini yaliyo kwenye makinikia, pamoja na hasara ambayo Serikali imekuwa ikipata kutokana na usafirishaji wa mchanga huo nje ya nchi, ziliibua madudu mengi ambayo sasa yamezaa mazungumzo kati ya Barrick na Serikali.
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeshaipa migodi iliyo chini ya kampuni hiyo deni la Sh trilioni 424, ikiwa ni makisio ya kodi iliyokwepwa pamoja na faini, kutokana na udanganyifu kwenye kusafirisha mchanga huo.
Wakati kwenye dhahabu hali ikiwa hivyo, katika biashara ya tanzanite nako kwa muda mrefu kumetajwa kuwapo kwa ukwepaji mkubwa wa kodi na madini hayo kusafirishwa nje ya nchi kwa njia za panya.
Hali hiyo ndiyo inayofanya kuwapo matarajio kuwa, Kamati ya Bunge ya kuchunguza biashara ya tanzanite, itakapomaliza kazi yake, kilio kilichopo kwenye kampuni ya dhahabu kitahamia pia kwa zile za tanzanite na wafanyabiashara wake wakubwa.
Tanzania inavyopoteza fedha
Mwaka 2014, aliyekuwa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja, alisema Tanzania haikufikia hata nusu ya Kenya kwa mauzo ya madini hayo ya vito.
Alisema mwaka 2013, Kenya ilisafirisha na kuuza nje ya nchi tanzanite ya dola milioni 100 za Marekani (Sh bilioni 173), huku Tanzania ikisafirisha za dola milioni 38 (Sh bilioni 45.5.
India iliuza Tanzanite ya Dola za Marekani milioni 300 (Sh bilioni 509).
Bila kumtaja jina, Kamishna huyo alisema mmoja wa wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka nchini Marekani aliwahi kumuuliza iwapo kuna migodi ya tanzanite India, kwa sababu akifika huko hupata tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya tanzanite inayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Manyara huuzwa kwa njia za panya nje ya nchi na kwamba Serikali imeanza kuchukua hatua.
Taarifa nyingine zinaonyesha kwamba, madini hayo ambayo hupatikana Tanzania pekee, huzipatia nchi mbalimbali duniani dola milioni 500 (Sh bilioni 800), wakati Tanzania ikibaki na kiasi kidogo tu cha fedha.
Wachimbaji wavaimia kamati
Juzi wachimbaji wadogo wa madini hayo wakiwa na mabango, walivamia ukumbi wa mikutano ambao Kamati ya Bunge ilikuwa inakutana na viongozi wao, na kupaza sauti zao juu ya wanavyodhulumiwa.
Walisema kwa miaka zaidi ya 10 iliyopita hawakuwa na tatizo, lakini tangu wawekezaji wazawa walipoinunua Tanzanite One, wamekuwa na migogoro isiyokwisha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara, Sadick Mnene, baada ya kukutana na kamati hiyo, alisema wameieleza matatizo yote kuhusu migogoro iliyopo.
Alisema wameiomba kupeleka kilio chao kwa Wizara ili iweze kutuma wataalamu wa miamba watakaofanya utafiti wa madini kwenye vitalu.
“Kwa sasa madini ya tanzanite yapo chini sana tofauti na miaka ya nyuma,” alisema Mnene.
Kwa upande wake Biteko, baada ya kuvamiwa na wachimbaji hao, aliwataka kuwa na imani na kamati hiyo, Bunge na Serikali na kwamba kazi ya Bunge ni kuhakikisha Serikali inawasaidia wachimbaji wadogo.
“Tumesikia mazungumzo yenu na mabango mliyoyashika yanaonyesha kuwapo kwa mahusiano mabaya na mwekezaji mkubwa jirani yenu, niwaombe sasa hivi tunakutana na viongozi wenu ndani kuzungumza tutawasikiliza. Kazi ya serikali ya awamu ya tano ni kuwasaidia nyinyi mfikie malengo.
“Tumekuja kuwasikiliza kwanza ili mkaendelee na shughuli zenu, kazi yetu sisi ni kuchunguza, kusikiliza kisha tutakwenda kuandaa ripoti maalumu itakayowasilishwa mbele ya Bunge. Niwahakikishie katika uchunguzi huu hakuna mtu atakayebaki salama,” alisema Biteko.
Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupitia mkataba baina ya Shirika la Madini la taifa (STAMICO) na Kampuni ya Tanzanite One, ikiwamo kuangalia ushiriki wa Kampuni ya Sky Associate na kwamba ni kwa namna gani serikali inanufaika na mkataba huo ama kupata hasara.
Pia imetakiwa kuchunguza mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini hayo.
Kilichotokea kwenye makinikia
Kilichotokea kwenye Makinikia kinatarajiwa kutokea pia kwenye tanzanite, kwa sababu malalamikio ya sekta hizo mbili yanafanana.
Kabla ya Rais John Magufuli kuunda kamati mbili zilizochunguza makinikia, wasiwasi juu ya kuwapo udanganyifu kwenye biashara hiyo na kwamba nchi haipati mapato kama inavyotakiwa, ulikuwapo.
Hali hiyo pia ndivyo ilivyo kwenye tanzanite, ambapo, nchi za Kenya na India zinatajwa kufaidika zaidi kuliko Tanzania yenye madini hayo.
Moja ya Kamati za Rais, iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osoro, ambayo ni sehemu ya chachu ya kuundwa hiyo ya tanzanite, ilibaini kuwa Tanzania inapoteza matrilioni ya fedha kwenye biashara hiyo.
Akisoma ripoti ya kamati yake, Profesa Osoro alisema takwimu walizokusanya kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA), mwaka 1998 hadi Machi 2017, makadirio ya chini yanaonyesha makontena yaliyosafirishwa nje ya nchi ni 44,277, huku kwa makadirio ya juu yakiwa 61,320.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh trilioni 132.56, sawa na dola bilioni 60.25 au Sh trilioni 229.9, sawa na dola za Marekani bilioni 104.5 kwa kiwango cha juu.
“Thamani ya madini yote katika makontena 61,320
yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh trilioni 183.597, sawa na dola za Marekani bilioni 83.45, kwa kiwango cha juu ni sawa na Sh trilioni 380.499, ambazo ni dola za Marekani bilioni 144.77,” alisema Profesa Osoro.
TRA na makinikia
Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo, TRA ilipeleka deni la kodi kwa migodi ya Bulyanhulu na Pangea, ambayo inaendeshwa kwa ubia na Acacia na Barrick yenye hisa asilimia 63.9
Katika kodi hiyo, Bulyanhulu inadaiwa kodi ya kati ya mwaka 2000 hadi 2017 na Pangea inadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, iliyochapishwa kwenye tovuti ya kampuni ya Acacia, kodi hiyo imetokana na ripoti za kamati mbili za Rais, zilizoonyesha kuwa wamekuwa hawatangazi kiasi halisi cha mapato yao yatokanayo na makinikia.
Uchambuzi huo wa TRA umeonyesha Mgodi wa Bulyanhulu unadaiwa dola za Marekani bilioni 154 (Sh trilioni 344.8) na Mgodi wa Pangea dola bilioni 36 (Sh trilioni 76.1).
Inasema dola bilioni 40 (Sh trilioni 89.5) ni malimbikizo ya kodi na dola bilioni 15 (Sh trilioni 335.9) ni adhabu na riba.
No comments:
Post a Comment