Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Urais na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC), Rais Mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametoa ujumbe wake kwa aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.
Ujumbe wa Kenyatta kwa Raila umekuja wakati ambapo mwanasiasa huyo ameendelea kushikilia msimamo wa kupinga matokeo yanayotangazwa na IEBC akidai kuwa yalichakachuliwa na kwamba mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu ulidukuliwa.
Akitoa hotuba yake baada ya kutangazwa rasmi kuwa mshindi, Kenyatta alimtaka Raila afahamu kuwa bado anahitaji kushirikiana naye katika kazi na kwamba hana uadui naye kwani wote lengo lao ni kujenga Taifa moja la Kenya.
“Tutafanya kazi pamoja, tutakua pamoja, tutaliendeleza hili taifa pamoja na tuko hapa tayari kuendelea kufanya mazungumzo na midahalo pamoja ili tuweze kujenga hili taifa letu pamoja,” alisema Kenyatta.
Aliongeza kuwa katika kila mashindano lazima kuna watakaoshinda na wale watakaoshindwa, hivyo anawapongeza walioshinda hata kutoka kambi ya upinzani na kwa wale walioshindwa wataendelea kushirikiana pamoja bila kujenga uadui.
IEBC ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa muhula wa pili akiwa na kura zaidi ya milioni nane (asilimia 54.27) dhidi ya Raila aliyepata zaidi ya kura milioni sita (asilimia 44.7).
No comments:
Post a Comment