Kigoma. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk Amani Kaborou amesema ndani ya chama hicho kuna watu ambao hawajaukubali mfumo mpya wa uchaguzi unaozuia vitendo vya kupanga safu na hivyo kuibua malalamiko katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Kigoma wiki iliyopita, Dk Kaborou alisema matatizo mengi wanayokumbana nayo katika uchaguzi huo yanatokana na hali hiyo.
Akifafanua maana ya kupanga safu, alisema ni vitendo vya baadhi ya viongozi kutoa fomu kwa watu wanaotaka wagombee au kuwanunulia kadi za uanachama watu wengi ili baadaye waweze kuwachagua.
Alisema katika utaratibu huo, baadhi ya viongozi huficha fomu na kuwapa wagombea wao.
“Matatizo tunayokumbana nayo katika uchaguzi yanaweza kusemekana yanaanzia na uchaguzi huu, kwa kuwa umekataza kabisa kabisa kupanga safu, yaani kuteua watu ambao baadaye watakuja kukupigia kura wewe katika awamu yako,” alisema.
Alisema kuna mahali ambako watu au viongozi wa kata hawakuwa tayari kuafiki utaratibu mpya wa chama na pale walipojaribu kuuendeleza, wananchi wliwasilisha malalamiko yao ngazi za wilaya hadi mkoa.
“Hilo la safu kwa kweli naona watu wengi walikuwa hajaliafiki, wanasema nini bwana! Naona hilo limekuwa kila mahali tangu ngazi ya tawi na kata,” alisema Kaborou aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema na mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho.
Akikataa kuingia kwa undani kwa kuwa vikao havijayajadili, Dk Kaborou alisema, “Wanachama wamesema kabisa, ‘tulikuwa tunapangwa na viongozi’ na wanashangaa utaratibu wa uchaguzi safari hii kwamba mtu anajichukulia fomu mwenyewe.”
Alisema katika chaguzi zilizopita, kuna wakati ilikuwa inatokea mtu anajikuta akigombea peke yake ana anapita kwa sababu wengine wamenyimwa fomu.
Hata hivyo, alisema safari hii mambo ni tofauti na kuna sehemu katika mkoa huo wa Kigoma ambapo mtu aliyegombea peke yake amepigiwa kura nyingi za hapana.
“Siwezi kutaja ni eneo gani kwa kuwa sina takwimu kamili hapa, lakini yupo. Hata hapahapa jana kwenye Jumuiya kuna mgombea kapata kura moja, fikiria katika mkutano wa watu 40 unapata kura moja,” alisema.
Alipoulizwa endapo kuna mahali wanachama hawakujitokeza kwa kuhofia utaratibu mpya, Dk Kaborou alisema awali hilo lilikuwapo, lakini baada ya elimu kutolewa, wengi wamejitokeza na sasa kuna ushindani mkubwa mkoani humo.
Mwenyekiti huyo ambaye anawania tena nafasi hiyo, alisema hana uzoefu wa kupanga safu na hivyo suala hilo halimsumbui.
“Hili halinipi shida, mimi sina uzoefu wa kupanga safu. Kwani nilipoingia hapa nilikuwa na safu gani. Na sasa hivi wamejitokeza watu 12 kuwania uenyekiti,” alisema.
Kuhusu nafasi ya wasaliti katika uchaguzi huo, Dk Kaborou alisema Mkoa wa Kigoma ulikuwa wa kwanza kuwaengua wanachama wanaodaiwa wasaliti na viongozi wasiopungua 50 walitimuliwa.
Alisema wengine walikata rufaa na kurudishwa, akitoa mfano wa kiongozi mmoja wanawake ambaye alirudishwa na halmashauri kuu lakini walio wengi hawakurudi.
Akifafanua aina ya usaliti waliofanya wanachama hao, Dk Kaborou alisema ilikuwa ni kusaidia upinzani, hasa chama cha ACT-Wazalendo ambacho kilishinda ubunge Kigoma Mjini na viti vingi vya udiwani.
No comments:
Post a Comment