WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amekuwa miongoni mwa wachezaji wa Difaa Hassan El- Jadida waliotumika kutambulisha jezi za msimu mpya za timu hiyo kabla ya baadaye kuingia uwanjani kuiongoza timu hiyo kushinda 2-1 dhidi ya ASO Daraja la Kwanza.
Msuva amesema kwamba katika mchezo huo uliofanyika wa El Abdi mjini Jadida, yeye amefunga bao moja ambalo lilikuwa la kusawazisha na kuseti la ushindi.
“Tumeshinda mabao 2-1, maana huku kila siku tunacheza mechi, kweli wenzetu wapo tofauti sana,”amesema Msuva na kuongeza; “Leo mimi nimefunga la kusawazisha na kutengeneza la ushindi,”.
Msuva amesema mechi zote wanazocheza za kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola dhidi ya timu tofauti, zikiwemo za Daraja la Kwanza ni ngumu.
“Ni mechi ngumu, timu za huku wachezaji wake wapo fiti sana na wana nguvu na kasi sana, kwa kweli huku wenzetu wapo tofauti sana,”alisema.
Awali ya hapo, Msuva alishiriki zoezi la kutambulisha jezi mpya za Jadida za msimu ujao pamoja na wachezaji wenzake wengine watatu walioteuliwa.
Zoezi jilo lilifanyika katika mkutano na Waandishi wa Habari mabao makuu ya klabu. Ikumbukwe ni wiki iliyopita tu Msuva amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na DHJ kutoka Yanga ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment