Askofu Josephat Gwajima.
MTIKISIKO mkubwa umetokea kufuatia bomoabomoa inayoendelea jijini hapa ambayo imeacha vilio kwa baadhi ya watu, huku ikibainika kuwa makanisa 20 na misikiti 11, ni miongoni mwa majengo yaliyowekewa alama za X kuashiria kuwa yatabomolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kupisha ujenzi wa Barabara ya Morogoro-Dar.
Uwazi lilifanya uchunguzi kuanzia eneo la Ubungo, Kimara, Mbezi Luis hadi Kiluvya jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita na jana na kubaini kuwa licha ya watu wa kawaida, waumini wa makanisa na misikiti hiyo wamejawa na simanzi kutokana na kukumbwa na bomoabomoa hiyo.
TANESCO WAKATALIWA KUKATA UMEME
Jana waandishi wetu walishuhudia baadhi ya wananchi wakiwakataza mafundi wa Tanesco kukata umeme kwenye baadhi ya nyumba ambazo zimewekewa alama X eneo la Kimara Stop Over, hata hivyo, hakuna aliyekuwa tayari kusema sababu za kufanya hivyo.
Kanisa la Ufufuo na Uzima.
MAKANISA YENYE ALAMA YA X
Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Maji, ni miongoni mwa nyumba za ibada zilizowekewa alama ya X, hivyo kiongozi huyo kukutwa na dhahma nyingine.Kiongozi huyo amekuwa akikumbwa na matukio mengi huku akifikishwa polisi na mahakamani mara kadhaa.
Katika uchunguzi wa gazeti hili, imebainika kuwa makanisa mengine yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni Kanisa la Anglikana Stop Over, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, KKKT Usharika wa Mbezi Luis, Kanisa Katoliki Kimara litakalobomolewa nusu, Kanisa Katoliki la Mbezi Luis, The River Healing Ministry of Tanzania la Kibamba na Kanisa la Calvary Salvation lililopo Kibamba.
Makanisa mengine ni Kanisa la TAG Rejoice Center la Mbezi, Kanisa la Kaprenan lililopo Kibamba, TAG – Suka, Pentekoste of Tanzania Kiluvya, Nayoth Church Kiluvya, KLPT la Bwawani, Kapernan Centre Mbezi, TAG Calvary Temple Mbezi Inn na GRC Mbezi Inn.
Shehe Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
MENGINE YAMEBOMOLEWA
Katika uchunguzi wetu, baadhi ya makanisa yameshabomolewa kutii agizo la kubomoa kwa hiyari likiwemo la Moravian Kimara Stop Over na KKKT Kibamba.
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Jumamosi iliyopita alikwenda kuwafariji na kuwatia moyo waumini wa kanisa lake ambao wamepatwa na simanzi kutokana na uamuzi huo wa serikali.
“Najua mna huzuni, majengo mengi yatabomolewa na serikali ili kupisha ujenzi wa barabara, kwa hili hamna budi kukubali na kuamini kuwa hiyo ni baraka kwa Mungu, zaidi kuweni na amani, ombeni baraka na kumshukuru Mungu,” alisema Dk. Malasusa.
Kwa upande wake, Mchungaji wa KKKT Kibamba, Mshiu Wilness alisema kanisa limepokea agizo la kutakiwa kuhama na kubomoa jengo hilo na kwamba, tayari wameshapata eneo jingine ambalo wanatarajia kuhamia.
“Tumepokea, tunatarajia kuondoka na tutavunja kama tulivyoelekezwa,” alisisitiza kiongozi huyo.
Msikiti.
MISIKITI NAYO YAKUMBWA
Licha ya makanisa hayo, kuna misikiti itakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ambayo ni Masjid Kilumbi Islamic Center – Kimara Mwisho, Dalul Mustafah wa Kimara Stop Over, Masjid Baitul Maamur, Masjid Jaaria, Al Masjid Nuur uliopo Kiluvya, Masjid Jaalia Gogan, Masjid Nuur Kibamba CCM na misikiti mingine mitatu ya Mbezi Inn, Mbezi Luis na Temboni.
VIONGOZI WA DINI WANENA
Wakizungumzia bomoabomoa hiyo, baadhi ya mashehe na wachungaji wametaharuki, wakisema wamepokea maagizo ya serikali ya kutakiwa kuvunja majengo yao huku wengine wakimuomba Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwatazama kwa jicho la huruma.
Imamu wa Msikiti wa Jamsjid Jaria wa Kiluvya, Haidary Masenga alisema waumini wameathirika kisaikolojia kwa kutojua msikiti huo utakakohamishiwa kwa kuwa hakuna eneo walilopata.
“Wote tunataka maendeleo na sisi hatupingi, lakini tunaomba tutazamwe kwa jicho la huruma tuachwe tuendelee kuabudu hapa. Mpaka sasa hatujui chochote tunasubiri tu hatima ya serikali kama watavunja au la,” alisema Imamu Masenga.
Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Kilumbi Islamic Center, Halfan Malima alimuomba Rais Magufuli kuwahurumia kwa kuwapa eneo lingine la ibada kwa kuwa bado hawajapata.
Mchungaji wa Kanisa la The River Healing Ministry of Tanzania, John Kyashama alisema anaunga mkono agizo la serikali la kubomoa nyumba, makanisa na misikiti ili kupisha upanuzi wa barabara.
Kyashama alisema hana kinyongo na rais na anaunga mkono mipango ya maendeleo anayoifanya na anawashauri wachungaji wenzake waliokumbwa na bomoabomoa kukubaliana na hali hiyo kwa kuwa kinachofanywa na serikali ni kwa nia njema.
“Si vizuri kuwa na kinyongo wala kuzozana na utawala, kila mtu atii mamlaka za nchi,” aliasa mchungaji huyo.
MALALAMIKO YA WANANCHI
Licha ya nyumba hizo za ibada, baadhi ya majengo ya wananchi pia yamewekwa alama ya X ambapo wengi wameitupia lawama serikali kwa madai kwamba wakati wanajenga nyumba hizo, walikuwa hawajavunja sheria yoyote.
Mzee John Mlangi (74), mkazi wa Kimara Stop Over alisema amejenga nyumba yake miaka 35 iliyopita na wakati huo hakukuwa na sheria ya ardhi aliyoivunja kwa kuwa alikuwa nje ya mita 60 kutoka kwenye barabara na kiwanja hicho alikuwa akikilipia kodi kwa miaka yote hiyo.
“Kutokana na kuwekewa alama ya X nimekuwa nikiishi kwa wasiwasi na nimepata ugonjwa wa shinikizo la damu,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stop Over, Kimara, Magreth Msabuso alisema katika mtaa wake, wapo wazee wengi waliostaafu ambao ikiwa nyumba zao zitabomolewa bila fidia, hali zao zitakuwa mbaya.
Alisema wananchi wote waliowekewa alama za X nyumba zao walipaswa kushirikishwa tangu hatua ya kwanza kabla ya kuweka alama hizo.
POLISI NAO WAKUMBWA
Mbali na nyumba hizo za kiraia na za kidini, pia Kituo cha Polisi Mbezi Luis kitabomolewa huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne akisema kilijengwa kwa nguvu za wananchi kutokana na mahitaji ya eneo hilo.
Alisema kutokana na kuwekwa alama ya X, kituo hicho kitahamishiwa eneo la Gogoni kwa kuwa licha ya kuwa barabarani, bado eneo lake ni dogo.
“Kituo hiki kitaondolewa hapa na kupelekwa kwenye kituo kingine cha Gogoni kilichojengwa chini ya mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na ujenzi wake umeshirikisha nguvu za wananchi na ni kikubwa kwa Wilaya ya Ubungo,” alisema.
VITUO VYA MAFUTA NAVYO BALAA
Vituo vya mafuta navyo vimekumbwa na balaa hilo na vilivyowekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa ni Camel Oil-Kimara Stop Over, Henry Filling Station-Mbezi kwa Yusuph, Camel Oil – Kibamba, Uduru Oil Station – Kibamba na Total-Stop Over.
HUDUMA ZA AFYA ZAKUMBWA
Vipo pia vituo vya huduma za afya vitakavyoguswa na bomoabomoa hiyo ambavyo ni Hospitali ya Boch na Kituo cha Afya cha Kimara vitakavyobomolewa nusu, Hospitali ya Neema iliyopo Kimara Stop Over, Kimara Centre Dispensary na Zahanati ya Arafa.
No comments:
Post a Comment