Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na hatua zinazochuliwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji dhidi ya watu waliouziwa viwanda na kisha kuvitelekeza na amemtaka Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Charles Mwijage kuvinyang’anya na kuwapatia wawekezaji wanaoweza kuviendeleza.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi kabla ya kufungua kiwanda cha kuzalisha saruji cha Kilimanjaro kilichopo katika eneo la Maweni Mjini Tanga ambako leo ameendelea na ziara yake ya siku 5 Mkoani Tanga.
Mhe. Rais Magufuli amesema nchi nzima ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo Mkoani Tanga lakini anashangaa kuona Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji havinyang’anyi licha ya kutoa maelekezo ya kufanya hivyo mara kadhaa.
Mhe. Rais Magufuli pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa katika maeneo yao ili kubaini ambavyo havifanyi kazi na kutafuta wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha.
Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro kina uwezo wa kuzalisha tani 300 za saruji kwa siku na kinatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 3,000 kwa siku mwaka ujao.
Baada ya kufungua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga Fresh) ambacho kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 50,000 kwa siku hadi kufikia lita 120,000 hatua ambao inatarajiwa kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa asilimia 42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi unaofanywa utaongeza uwekezaji kutoka Shilingi Bilioni 12 hadi kufikia Shilingi Bilioni 26.5.
Akiwa kiwandani hapo Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukabidhi hati miliki ya kiwanda hicho kwa menejimenti ya kiwanda, na ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyokuwa ikidai kodi ya ongezeko la mtaji kuelekeza madai hayo kwa mmiliki wa awali wa kiwanda hicho aliyewauzia wakulima.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage kuchukua hatua dhidi ya kiwanda cha maziwa cha Arusha ambacho baada ya kubinafsishwa kimegeuzwa kuwa kituo cha kukusanyia maziwa na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kusindikwa.
Pia amemuagiza Waziri Mwijage kuwa nchi yoyote itakayozuia maziwa ya Tanzania nayo izuiwe kuingiza maziwa yake hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvivu Dkt. Charles Tizeba kufika kiwandani hapo na kushughulikia changamoto zinazokikabili kiwanda hicho.
Mhe. Rais Magufuli amefungua awamu ya kwanza ya mradi wa kituo cha matanki ya mafuta cha GBP kilichopo katika eneo la Raskazone Mjini Tanga ambacho kina uwezo wa kuhifadhi lita Milioni 122.6 na ambacho kinatarajia kupanuliwa hadi kufikia lita Milioni 300 ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa GBP Bw. Badar Sood kwa uwekezaji huo mkubwa wa Shilingi Bilioni 60 utakaojumuisha ujenzi wa kiwanda cha vilainishi na kiwanda cha kusindika gesi na amemhakikishia kuwa Serikali itaendelea kumuunga mkono wakati wowote.
Pia Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Sood kwa kulipa kodi ipasavyo ambapo katika mwaka miaka miwili iliyopita ameongeza malipo ya kodi kutoka Shilingi Bilioni 208.950 hadi kufikia Shilingi Bilioni 293.263 na amewahakikishia wawekezaji wote wanaolipa kodi ipasavyo kuwa wapo salama na Serikali itawalinda.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa mita za kupimia mafuta yanayoshushwa kutoka melini (Flow Meter) na ametaka Wizara zinazohusika katika mchakato huo kununua mita hizo haraka ili mafuta yanayoingia nchini yapimwe kwa usahihi na kukusanya kodi stahili.
Kesho Rais Magufuli atahitimisha ziara yake Mkoani Tanga kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni.
No comments:
Post a Comment