Mamia ya watu wenye Ulemavu wa Miguu wamejitokeza kwa wingi leo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuchukuwa vipimo kwaajili ya kupatiwa Miguu bandia ambapo idadi imekuwa kubwa tofauti na ilivyo tarajiwa huku wengine wakitokea Mikoani.
Mwitikio huo ni kufuatia Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kuwatangazia wenye uhitaji ya Miguu Bandia kufika ofisini kwake kwaajili kuchukuliwa vipimo ili wapatiwe miguu hiyo bila malipo ambapo hadi saa nne asubuhi walemavu waliokuwa wamefika ni zaidi ya 500.
Makonda amesema licha ya idadi hiyo kuzidi ile ya watu 200 iliyokusudiwa atahakikisha wote wanapimwa na wataalamu na kupatiwa huduma bila ubaguzi wa Mikoa wanayotoka sababu wananchi wote wapo chini ya Rais Dr.Magufuli.
Amesema wote watakaopimwa watatengenezewa Miguu yao kulingana na vipimo vilivyochukuliwa.
Hata hivyo Makonda amesema kutokana na wingi wa watu wenye uhitaji ataongeza siku za upimaji na kuongeza idadi ya wataalamu ili wote watakaofika wahudumiwe.
Aidha amesema awamu hii ya kwanza walemavu 200 watapatiwa miguu ya bandia wakati akiendelea kufanya jitiada za kuwasiliana na wadau ili waweze kuchangia na kuhakikisha wananchi wote wanahudumiwa.
Mbali na miguu bandia pia Makonda amefanikiwa kupata Magongo ya kisasa 17 kutoka Nchini Marekani ambayo pia atayatoa bila malipo kwa wale wenye uhitaji.
No comments:
Post a Comment