Sungo blog
CHAMA cha Act-Wazalendo kimesikitishwa na kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa jana kwenye ufunguzi wa mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kuhusu mishahara ya wafanyakazi aliposema alipoingia madarakani hakusema ataongeza mishahara kwa vile hakuchaguliwa kuongeza mishahara na kwamba ana jukumu la kuwahudumia wananchi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema:
“Swali la kujiuliza baada ya kauli hiyo ni, je, wafanyakazi wa Tanzania wanastahili kufanyiwa hivi na serikali wanayoihudumia? Jibu bila shaka ni hapana. Serikali inatoa wapi ujeuri wa namna hii dhidi ya wafanyakazi nchini wakati kiuzalishaji na kimapato inawategemea wafanyakazi?
“Licha ya mchango wao madhubuti katika ujenzi wa taifa kwenye sekta mbalimbali, kwa utumishi wao wa kutukuka, ukweli wa mambo ni kuwa wafanyakazi ndiyo wanaochangia zaidi mapato ya serikali kuliko waajiri wao.
“Kwa mfano, kitabu cha mapato cha mwaka 2016/17 kinaonyesha kuwa wafanyakazi wote wa sekta ya umma na sekta binafsi watachangia jumla ya Sh. Trilioni 3 kwenye mapato yote ya serikali kulinganisha na wenye mitaji (waajiri) ambao watachangia jumla ya shilingi bilioni 900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la mitaji na riba.”
“Ni kwa nini serikali inawadharau na kuwahadaa wafanyakazi? Wakati wa kampeni za kugombea urais, Magufuli alijipambanua mbele ya Watanzania kuwa akichaguliwa kuingia madarakani, serikali itahakikisha kuwa inasimamia maslahi bora ya wafanyakazi ikiwemo mishahara bora,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment