Breaking




Monday, 9 October 2017

HIKI NDIYO KITU KINACHOSABABISHA KUONA MAISHA YAKO NI MAGUMU NA HAYANA MAANA

Sungo blog

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza kitu kinachosababisha kuona maisha yako ni magumu na hayana maana hapa duniani. Je unajua ni kitu gani hicho? Karibu tujifunze.

Ndugu msomaji, muda mwingine tunajiona hatuna maana katika maisha yetu, hatuna furaha na tunaona mambo ni magumu sana. Jamii imekaririshwa kulalamika na kuishi maisha ya hofu ambayo yanapelekea watu kukata tamaa ya maisha. Watu wanajiona hawana wanachofanya katika maisha yao kwa sababu ya kushindwa kuishi wakati wa sasa na kujifananisha na maisha ya watu wengine.

Rafiki, kama tukianza kujiuliza swali hili lifuatalo ndipo tunapoanza kuona kweli maisha ni magumu kwako na wala hayana maana. Swali ambalo ni sumu na baya kujiuliza katika maisha yako ni NIMEKOSA NINI MIMI? Hakika ukianza kujiuliza umekosa nini itakuwa ni litania ndefu ya majibu ambayo yatakufanya kujiona wewe huna unachofanya katika maisha yako.

Jamii ya leo imekosa shukrani watu wanaanza kujiuliza kuwa wamekosa kitu gani katika maisha yao badala ya kushukuru walivyonavyo. Maisha ni magumu sana kama ukianza kujiuliza umekosa nini katika maisha yako kwa sababu swali hili haliwezi kukuacha salama. Utaanza kujilinganisha na wengine huna kitu fulani na mwenzako anacho hapo sasa ndipo watu wanaona maisha yao hayana maana. Wengine wanalalamika wanafanya kazi lakini mshahara mdogo lakini kumbuka wakati wewe unalalamika mshahara mdogo kuna mwingine anatamani hana kazi anatamani apate hata hiyo ya mshahara mdogo.

Ukipoteza shukurani katika maisha yako umepoteza fadhila zote. Watu wanapenda kujiangalia wamekosa nini badala ya kushukuru kwa kile ambacho wanacho katika maisha yao. Kuwa hai tu ni jambo la kushukuru Mungu kwa sababu kuna wengine wameshakufa na walitamani waendelee kuishi hapa duniani ila unakuta mtu analalamika kwa kukosa shukrani. Usihesabu vile ambavyo huna bali hesabu vile ambacho unavyo.

Rafiki, kukosa kushukuru kwa vile ambavyo tunavyo ndiyo sababu ya watu wengi kuona maisha yao hayana maana yaani hakuna kitu wanachofanya hapa duniani. Kama uko mzima shukuru kwa sababu uko mzima kwa sababu kuna mwenzako ni mgonjwa anatamani kuwa mzima kama wewe, kama unaumwa usilalamike kwa sababu kuna mwingine yuko hospitalini anakata roho. Usilalamike umekosa kitu fulani bali shukuru kwanza kwa chochote kile ambacho Mungu amekujalia kuwa nacho katika maisha yako.

Utawezaje kuwa na furaha katika maisha yako kama wewe ni mtu ambaye huna shukurani? Unajiuliza umekosa nini katika maisha badala ya kujivunia kwanza kwa kile ambacho unacho sasa? Ukianza kujiuliza umekosa nini utapata vitu vingi ambavyo hukutegemea hatimaye vinakupelekea wewe kudharau maisha yako na kuona maisha ya wengine ndiyo yana thamani kubwa. Utaanza kuona maisha yana thamani pale utakapoanza kujikubali na kushukuru kwa kile ambacho unacho. Ukianza kushukuru utafungua mlango wa baraka wa kupata vile ambavyo huna na utajiona maisha ni mazuri kuliko kudharau kile ambacho unacho sasa na kukiona hakina maana kwako.

Hatua ya kuchukua leo, usijiulize umekosa nini katika maisha yako. Shukuru kwa kile ambacho unacho sasa ndiyo utaweza kuyaona maisha yako yana baraka na mazuri lakini ukishayadharau maisha yako kwa sababu ya kuona huna kitu fulani utajikuta uko katika hali ngumu sana.

Kwa hiyo, maisha ni furaha. Kuwa na shukrani katika maisha yako badala ya kuanza kujidharau maisha yako kwa kujiuliza umeanza kukosa nini. Ushindi wowote mdogo unaopata katika maisha ni jambo la kushukuru sana kwa sababu kile unachopata wewe na unakidharau kuna mwingine hana. Shukuru kwa kila jambo katika maisha yako.

No comments:

Post a Comment