Sungo blog
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro amewataka wananchi wenye taarifa kuhusu alipo mtu aliyemtolea bastola hadharani Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wafanye hivyo.
IGP Sirro leo Jumatano akiwa ziarani mkoani Mtwara amesema mtu huyo alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.
Amesema kuonekana kwa picha za mtu huyo haina maana kwamba atapatikana kwa urahisi hivyo jeshi hilo linaendelea kumtafuta.
“Mheshimiwa Nape amefungua kesi. Ujue picha kuonekana haina maana kwamba yule mtu ataonekana kirahisi lakini upelelezi unaendelea kumtafuta aliyefanya tukio hilo. Wananchi watusaidie, maana suala la kumpata mhalifu ni ushirikiano, sisi tunaenda kwa taarifa, bila taarifa ya uhakika hatuwezi kufanikiwa,” amesema.
Akizungumzia uhalifu wilayani Kibiti, IGP Sirro amesema baadhi ya watuhumiwa wamekimbilia mkoani Mtwara na wataendelea kuwashughulikia.
Amewataka wanaojihusisha na uhalifu yakiwemo mauaji ya raia kuacha vitendo hivyo alivyoviita vya hovyo. Amesema kukimbia hakuwasaidii badala yake waache na kuwa raia wema.
“Kuna changamoto, waliokuwa Kibiti nasikia baadhi yao wamekimbilia huku na bahati nzuri tuna vijana wetu pia wameingia hapa,” amesema.
IGP Sirro amesema, “Niliwaambia hakuna salama yao katika Tanzania labda wakimbilie sehemu nyingine, lakini Mtwara bado iko Tanzania na ukienda Lindi bado iko Tanzania, tutawapata huko waliko na tutawagonga vizuri kwa mujibu wa sheria kwa sababu wao ndio wameanzisha ligi. Ukianzisha ligi jitahidi kumaliza ligi sasa kumaliza ligi si kukimbilia Mtwara.”
No comments:
Post a Comment