Sungo blog
Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 na majeruhi 9 baada ya lori aina ya Fuso lililoanguka katika eneo la Ntembwa ndani ya hifadhi ya Lwafi Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.
Ajali hiyo imetokea jana tarehe 03 Oktoba, 2017 majira ya saa 2 usiku baada ya lori aina ya Fuso linalomilikiwa Bwana Bakari Kessy ambaye ni mtoto wa mbunge wa Nkasi Kaskazini Ally Keissy Mohamed.
Kufuatia ajali hiyo Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelothe Stephen, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na vifo hivyo.
“Natambua hiki ni kipindi kigumu kwa wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii, natambua kuwa wamepoteza wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea, nawapa pole sana kwa kufiwa na naungana nao katika maombi ili roho za marehemu zipumzishwe mahali pema peponi, Amina” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili warejee katika afya njema na kuungana na familia zao katika maisha yao ya kila siku.
Mbali na hilo Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana zaidi na matukio ya ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali zao.
No comments:
Post a Comment