Breaking




Monday 9 October 2017

MSUKUMA ADAI WANAWEZA WASIOMBE HELA KWA RAIS KWA MIAKA 29

Sungo blog

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Geita, Joseph Kasheku Msukuma amesema kuwa endapo watashinda kesi dhidi ya mgodi wa GGM ambayo wameifungua, watakuwa na uhakika wa kupata fedha ambazo zinaweza kuhudumu katika halmshauri kwa miaka 29, bila kuomba kwa Rais fedha yoyote.

Msukuma ambaye pia ni Mbunge wa Geita amesema hayo alipokuwa kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM katika Wilaya ya Geita ambapo alitumia nafasi hiyo kuwataka madiwani wa CCM wote ambao wanahitajika kituo cha polisi waende polisi wenyewe wakahojiwe na kuwaambia siku ya kwenda mahakamani wavae sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nitumie fursa hii kuwaomba madiwani wote wa CCM wa Geita Mjini, Geita na wale wa Busanda ambao tulikuwa kwenye kikao kile jitokezeni, muende wenyewe polisi, msikimbie nendeni wote polisi na tarehe 9 na 10 tunaenda mahakamani na sare za CCM, na mimi kamanda wenu nawaambia kuwa tutashinda tumeweka mawakili tisa. Dola milioni 12 ni sawa na bilioni 29, halmashauri kama ya Geita peke yake huwa tunatumia bilioni 1.5 mpaka 1.8 maana yake wakitulipa hizo hela tunaweza kuwa na miaka 29 bila kumuomba Rais hela,”alisema Msukuma.

Mbunge Msukuma pamoja na madiwani kadhaa wa CCM waliingia katika misukosuko wiki kadhaa zilizopita baada ya kukamatwa na jeshi la polisi na kulazwa ndani kwa masaa 24 kwa kile kilichoeleza kuwa walihusika katika kufanya vurugu kwenye mgodi wa Geita Gold Mine na kufunga barabara inayoingia mgodini huko wakishinikiza malipo hayo ya Dola milioni 12.

No comments:

Post a Comment