Breaking




Monday 9 October 2017

MWIGULU NCHEMBA AZIVAA TAASISI ZINAZOTOA RIPOTI YA UONGO KUHUSU WAKIMBIZI WA BURUNDI

Sungo blog

Sakata la wakimbizi kurudi nchini mwao ambalo limeendelea kubadilishwa badilishwa kimtazamo na baadhi ya mashirika ya kimataifa, limetua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliyesisitiza kuwa halijasitishwa.

Nchemba amesema kazi ya kuwaandikisha wakimbizi wa Burundi wanaotaka kurejea kwao kwa hiari haijasitishwa licha ya baadhi ya mashirika ya kimataifa kudai usalama wa wale wanaorudishwa uko hatarini.

Hivi karibuni shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu la Amnesty International lilidai kwamba mpango wa kuwarejesha wakimbizi hao unahatarisha maisha yao na linaamini kuwa wengi wanarejeshwa kutokana na msukumo wa ushawishi kutoka Serikali za Tanzania na Burundi.

Shirika hilo lilidai kuwa hali ya usalama bado si shwari likieleza kuwapo kwa matukio ya utesaji, kufungwa bila makosa, kubakwa na hata kuuawa.

Hata hivyo, Mwigulu alionyesha kushangazwa na ripoti hizo akisema mawasiliano yake na waziri mwenzake wa Burundi yamethibitisha kutokuwapo kwa matukio ya aina hiyo.

“Sijui hizi ripoti wanazipata wapi, mimi nimezungumza na mwenzangu wa Burundi na amenithibitishia kuwa hali iko shwari na hakuna dhoruba zozote zinazowapata wakimbizi wanaorejea kwao.

"Wakimbizi wanaojiandikisha wameongezeka mara mbili kuanzia wale wa awali 12,000 na sasa wamefikia 24,000. Hawa wakimbizi wamethibitishiwa na ndugu zao kuwa hali nyumbani kwao ni shwari na ndiyo maana wanaendelea kujiandikisha,” alisema.

Mwezi uliopita, Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) walikubaliana kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wawe wamewarejesha wakimbizi 12,000 wanaoishi Tanzania ambao wanataka kurudi kwao Burundi kwa hiari.

No comments:

Post a Comment