Breaking




Monday, 9 October 2017

WAMAMA WALALAMIKA KUKIMBIWA NA WAUME ZAO MUHIMBILI

Sungo blog

Baadhi ya wanawake ambao wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwauguza watoto wao baada ya kubainika wana matatizo ya saratani, wamelalamika kukimbiwa na waume zao.

Wanawake hao walisema chanzo cha kukimbiwa ni baada ya gharama za matibabu na dawa za saratani kuwa ghali, ikilinganishwa na magonjwa mengine.

Akizungumza na gazeti hili juzi wakati wa kupokea misaada yenye thamani ya Sh3.3 milioni iliyotolewa jana na Lions Club kwa watoto wanaoishi na saratani, Gigwa Izunya (40) alisema tangu amelazwa hospitalini hapo na mtoto wake Holo Jika (2) hakuna ndugu aliyefika hivyo anaishi na kutibiwa kwa msaada wa Muhimbili.

“Nililetwa Muhimbili Aprili 14 kutokana na matatizo ya jicho la mwanangu ambayo imethibitishwa kuwa ni saratani, hakuna ndugu wala mume walionitembelea mpaka sasa Holo amewekewa jicho bandia,” alisema.

Gigwa, mkazi wa Dodoma ni kati ya wanawake wanaouguza watoto wao wanaosumbuliwa na saratani waliotelekezwa na ndugu.

Naye Rehema Athuman (29) kutoka mkoani Lindi, alilalamikia kutengwa na familia yake kwa miezi kumi sasa baada ya mtoto wake kugunduliwa na saratani ya ngozi.

“Alianza kwa kuvimba shavu na baadaye ngozi yake ikaanza kupata harara, alipokea matibabu ya muda mrefu bila mafanikio tulipofika Muhimbili tukaambiwa ni saratani, akalazwa tangu hapo nimetelekezwa nasaidiwa na kaka yangu mara moja moja anapita kutujulia hali,” alisema Rehema.

Mkufunzi wa Saikolojia wa Lions Club, Bhavika Sajan alisema klabu hiyo imeanzisha huduma ya kuwatia matumaini wazazi wanaouguza watoto wao kupitia Kituo cha Ujasiri House kilichopo hospitalini hapo.

Alisema gharama za matibabu na dawa za saratani vimeendelea kuwaumiza wagonjwa wa kipato cha chini, huku wakiendelea kuhitaji misaada ya wahisani mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo, Stella Rushagara ambaye alimwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema kuna changamoto ya matibabu kwa walio wengi.

“Hasa kwa wagonjwa wa saratani, wanatumia dawa ambazo ni ghali hivyo mkitusaidia dawa mtawasaidia zaidi wanaohangaika na matibabu,” alisema Rushagara.

Naye Naibu Gavana wa Lions Club, Mustafa Kundrat alisema misaada hiyo wameitoa katika kusherehekea huduma kwa jamii duniani, ambayo huadhimishwa Oktoba kila mwaka.

“Mwaka huu tumekuja Muhimbili tunataka kusherehekea kwa kutoa misaada kwa wagonjwa kupitia vitu mbalimbali vyenye uhitaji kwao,’’ alisema.

No comments:

Post a Comment