Miaka mitatu iliyopita, video ilitolewa ya kiongozi wa kundi linalojiita Islamic State (IS), Abu Bakr al-Baghdadi, akiwataka wapiganaji wa kundi hilo wamtii katika hotuba aliyoitoa katika msikiti mkubwa wa al-Nuri mjini Mosul.
Mji huo wa Iraq ulikuwa umetekwa tena na wapiganaji wa kundi hilo na wakatangaza dola ya Kiislamu.
Wakati huo, IS, walikuwa wanadhibiti eneo la ukubwa sawa na Uingereza, lakini tangu wakati huo muungano wa majeshi ya nchi mbalimbali duniani umewakabili wapiganaji hao na kupunguza sana maeneo wanayoyadhibiti.
Bado haijulikani alipo Baghdadi, ambaye Marekani wametoa zawadi ya $25m kwa atakayetoa habari za kusaidia kupatikana kwake.
Wakati huu ambapo ni miaka mitatu tangu kutolewa kwa hotuba ya kwanza hadharani ya Baghdadi, na yake ya mwisho, IS hawadhibiti tena maeneo ya ardhi ambayo walidhibiti awali na kiongozi huyo wao amesalia kimya tangu alipowahutubia kwa kanda ya sauti Novemba mwaka jana, baada ya vita vya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwa IS kuanza.
Kumekuwa kukitolewa taarifa za kifo cha Baghdadi siku za karibuni, huku kimya chake kikizidi.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi alisema kuna uwezekano mkubwa sana kwamba aliuawa kwenye shambulio la kutoka angani lililotekelezwa na wanajeshi wa Urusi mjini Raqqa tarehe 28 Mei.
Na afisa wa Iran alisema wiki iliyopita kwamba "bila shaka alifariki".
Hata hivyo, maafisa wa Marekani wametilia shaka madai hayo.
Kwenye video kutoka Raqqa wiki moja baada ya taarifa kutoka kwa Urusi, wapiganaji wa IS walizunmza kuhusu "sheikh wetu" bila kutaja jila la Baghdadi, na kuacha bado kukiwa na utata kuhusu hatima yake.
Si jambo la ajabu kwani Taliban na al-Qaeda pia walificha habari kuhusu kifo cha kiongozi wa Taliban Mullah Omar kwa miaka miwili.
Kwa wafuasi wake na maadui zake, ni jambo la kushangaza kwamba Baghdadi amesalia kimya.
'Mji mkuu wa tatu'
Jibu la kuhusu ni wapi Baghdadi yupo huenda likahusiana na madai yake kuhusu uhalali wake kama Khalifa au "kamanda wa waumini".
Kwa mujibu wa kanuni moja yeye utata wa kidini, mtu anaweza tu kujidai kuwa Khalifa iwapo ana "ardh tamkeen", au "ardhi ya kutawala".
Leo hii, ardh tamkeen inadidimia. IS kwa sasa ni kama karibu wameshindwa Mosul na pia wanashambuliwa vikali Raqqa, miji miwili ambayo wamekuwa wakiitumia kama miji mikuu yao Iraq na Syria.
Kama ishara ya kutambua utawala wao ulikuwa unakaribia kikomo Iraq, IS walilipua msikiti wa al-Nuri wiki mbili zilizopita kabla ya wanajeshi kuteka eneo hilo
Baghdadi huenda akawa mafichoni katika eneo ambalo limeelezwa kama "mji mkuu wa tatu wa IS", maeneo ambayo yanadhibitiwa na kundi hilo katika mpaka wa Syria na Iraq.
IS huita eneo hilo Wilayat al-Furat, au "Mkoa wa Euphrates", eneo ambalo linajumuisha mji wa Iraq wa al-Qaim na mji wa Syria wa Albu Kamal.
Mwaka 2014, IS walianza kwa kudhibiti Wilayat al-Furat na maeneo ya karibu.
Kwa mujibu wa kundi hilo, kupitia video walizotoa juzi kutoka mkoa wa Anbar nchini Iraq, wapiganaji hao walitumia eneo hilo kutekeleza mashambulio ya kasi sana Iraq na Syria.
Eneo hilo lina makundi ya wanamgambo na makuindi ya kikabila, ambayo yanaweza kuendelea kudhibiti eneo hilo hata baada ya kutekwa na wanajeshi kutoka kwa IS.
Hata katika maeneo yaliyokombolewa kama Rutba, mji ulio kusini, IS bado wameendelea kutekeleza mashambulio ya kuvizia.
MAFICHO JANGWANI
Hakuna operesheni yoyote ya kijeshi ambayo imeanzishwa kujaribu kukomboa miji hiyo ya mbali.
Mashauriano kuhusu iwapo ni wanajeshi wa Marekani na washirika wao wanaofaa kuongoza mashambulio upande wa Syria au wanajeshi wa serikali ya Syria bado yanaendelea Washington.
Iwapo Marekani ndiyo itaongoza mashambulio hayo, bado kuna maswali kuhusu iwapo wapiganaji waasi au wapighanaji wa Kikurdi wa Syrian Democratic Forces (SDF) ndio wanaofaa kuongoza mapigano hayo.
Nchini Iraq, maeneo kama vile Tal Afar, magharibi mwa Mosul, yanaonekana kupewa kipaumbele sana kwa sasa na wapiganaji wanaounga mkono serikali.
Hisham al-Hashimi, mshauri wa serikali ya Iraq ambaye pia ni mtaalamu kuhusu makundi ya wanamgambo nchini Iraqi, anasema kuna uwezekano mkubwa kwamba al-Baghdadi amejificha Wilayat al-Furat.
Wanajeshi wa Iraq wametekeleza mashambulio kadha ya kutoka angani eneo la Albu Kamal miaka miwili iliyopita.
Iyad al-Jamili, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa al-Baghdadi alionekana katika mji huo wa Syria, kwa mujibu wa Bw Hashimi.
Washirika wengine kadha wa karibu wa kiongozi huyo wa IS pia walionekana Albu Kamal na Mayadin, mji mwingine muhimu kwa IS katika mkoa wa Deir al-Zour nchini Syria, Bw Hashimi anasema.
Wilayat al-Furat ndio eneo pekee lililosalia ambapo IS wanaweza kusema kwamba wana ardh tamkeen.
Operesheni ya kijeshi ya kukomboa eneo hilo inaweza kuchukua miezi kadha kabla ya kuanza, na bila shaka muda hata zaidi kuikamilisha.
Hata baada ya maeneo hayo kukombolewa, IS wanaweza sana kutumia jangwa, mabonde ya mito na maeneo ya mipakani kama maficho kuteleza mashambulio mijini.
KUTAFUTWA SANA
Baghdadi, tofauti na viongozi wengine wa makundi ya Kiislamu, sana huzungumza au kuonekana hadharani wakati kuna haja kubwa sana ya kufanya hivyo - mfano alipokuwa anatangaza dola ya Kiislamu na wakati wa kutoa wito kwa wafuasi wake kupigania Mosul.
Unavyopanda juu kwenye vyeo miongoni mwa viongozi wa IS, ndivyo mawasiliano yanavyoendelea kupungua. Sana huwa kati ya watu wachache tu waaminifu.
Ni watu wachache sana wanaofahamu Baghdadi yuko wapi, jambo linalofanya vigumu kwa Marekani kujua yuko wapi kiongozi huyo anayetafutwa sana duniani.
Maeneo ya mpakani ya Syria na Iraq yanaweza kumpa Baghdadi eneo salama na analoweza kufahamu vyema, ambalo anaweza kujificha na kukwepa majaribio ya kumkamata au kumuua.
Aidha, yanampa uwezo wa kuendelea kudai kuwa kamanda wa waumini - kwa kuwa na ardhi anayoitawala.
Hassan Hassan ni msomi katika Taarisi ya Tahrir kuhusu Sera ya Mashariki ya Kati, Washington na ni mwandishi wa ISIS: Ndani ya Jeshi la Kutisha.
No comments:
Post a Comment