Breaking




Friday, 7 July 2017

POLISI WAFANIKIWA KUWAUA WAHALIFU WENGINE WAWILI HUKO KIBITI



 

Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwaua wahalifu wawili ambao ni miongoni mwa wahalifu wanaoendesha mauaji katika Kanda maalumu ya Polisi Rufiji kufuatia operesheni kali inayoendelea katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani. 

Akielezea tukio hilo, Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumatano Julai 5 majira ya saa nne usiku katika msitu wa Ngomboroni kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri Kanda maalumu ya Rufiji ambapo askari wa operesheni maalum wakiwa katika doria za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea katika Kanda hiyo ya kipolisi.

Sabas alisema Askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika mauaji hayo ambaye alikuwa amekamatwa na baada ya mahojiano alikubali kwenda kuwaonesha Polisi mahali ambapo ni maficho ya wenzake.

Sabas alieleza kuwa, baada ya kufika eneo la msitu wa Ngomboroni kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo askari Polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi naye alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili.

Majeruhi hao wawili walifariki dunia njiani wakati wakipelekwa hospitali kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na shot gun moja pamoja na risasi tisa za SMG zilizokuwa kwenye Magazine.” Alisema Sabas.

Aidha, mkuu huyo wa Operesheni maalum za Jeshi la Polisi Naibu kamishina Sabas ameendelea kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia na kwamba zawadi nono bado ipo pale pale na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wahalifu wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya Rufiji.

No comments:

Post a Comment