Breaking




Monday, 14 August 2017

WANAWAKE WILAYANI GAIRO WAJIFUNGULIA NYUMBANI KWA KUKOSA ZAHANATI




Wajawazito katika kijiji cha Kumbulu wilayani Gairo mkoani Morogoro kwa muda mrefu wamekuwa wakijifungulia majumbani na kuhatarisha usalama wa maisha yao na watoto au kulazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 25 kufuata huduma za afya vijiji vingine vya mbali wilayani humo na wakati mwingine kwenda wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma kutokana na kukosa kituo cha kutolea huduma za afya kwa muda mrefu.

Wakizungumza na ITV, wazee walioshi miaka zaidi ya 50 kijijini hapo wamesema hali hiyo imewasababishia wengi wa wanawake wajawazito kutegemea wakunga wa jadi kujifungua jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya mama na mtoto huku wengine wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya maeneo mengine ya mbali na kushukuru serikali kutambua mahitaji yao.

Kaimu mganga mkuu wilaya ya Gairo Amoss Aleluya amekiri kuwepo kwa changamoto ya kujifungulia nyumbani kwa wajawazito katika kijiji hicho na wamejipanga kuwaelimisha juu ya athari zake na umuhimu wa kuitumia zahanati huku mbunge wa jimbo la Gairo Ahmed Shabiby na viongozi wa halmashauri hiyo wakiwataka wananchi kuunda kamati maalum itakayosaidia kulinda dawa na vifaa tiba  dhidi ya watumishi wasio waaminifu.

No comments:

Post a Comment