Breaking




Sunday, 11 March 2018

KOCHA WA YANGA; TUKISHINDA KESHO SIMBA IJIANDAE

Sungo blog

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina amesema kuwa endapo kikosi chake kitaibuka na ushindi kesho Jumatatu dhidi ya Stand United, basi Simba ijiandae kukaa pembeni.

Habari za ndani ambazo Spoti Xtra imezipata kwa viongozi wa Yanga ni kwamba wamegomea rai ya baadhi ya wadau kutaka mchezo wao dhidi ya Stand uahirishwe kwa madai kwamba wanaucheza kwa mipango maalum.

“Makocha wamekataa kuahirisha mechi ya Stand kwa vile wanasema ni mkakati mzuri wa kukaa kileleni na kwenda sambamba na Simba kama Simba wameahirisha yao ni juu yao, makocha wanautumia huu mchezo kama mzuka wa kwenda Botswana,” alidokeza kiongozi mmoja wa Yanga. Aliongeza kwamba wanataka kufuta tofauti yao na Simba ili wakitoka kwenye michuano ya kimataifa wajue wamebaki na kazi moja tu ya kukomaa kileleni.


Yanga itapambana na Stand United kesho Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katika mchezo wa ligi na endapo itashinda itafikisha pointi 46 sawa na Simba inayoongoza msimamo wa ligi hiyo lakini itakuwa nyuma kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungumza na Spoti Xtra, Lwandamina alisema; “Mpaka tunafika hapa wengi walikuwa hawaamini kutokana na kuwa na majeruhi wengi, hata hivyo endapo tutashinda mchezo wa Jumatatu dhidi ya Stand United naamini kabisa tunaweza kuishusha Simba kutoka nafasi ya kwanza.”

“Ushindi huo, pia utasaidia kurudisha hali ya ushindani kwa wachezaji wangu lakini hamasa kwa wale ambao hapo awali walionekana kukata tamaa kama tunaweza kuwa mabingwa kwa mara nyingine tena, namuomba Mungu iwe hivyo hiyo Jumatatu katika mchezo huo,” alisema Lwandamina ambaye kiongozi mmoja wa Yanga alikiri kwamba angekuwa Kocha mzungu angeshatimka.


Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika alisema; “Tumejipanga vizuri na tunapambana vilivyo kuhakikisha tunaweka mambo sawa ndani ya timu ili kurudisha hali ya ushindani kwa wachezaji wetu ambayo hapo awali ilikuwa imepotea.”

“Lakini pia tunapambana kuhakikisha wachezaji wote waliokuwa majeruhi wanakuwa sawa baada ya kutoka Botswana kucheza mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Township Rollers, ili waweze kuongezea nguvu timu yetu katika harakati zetu za kuhakikisha tunaishusha Simba kutoka nafasi ya kwanza,” alisema Nyika. “Thabani Kamusoko tayari amerejea uwanjani, lakini pia Donald Ngoma naye muda si mrefu anarudi kwa hiyo mambo yatakuwa ni moto.”

No comments:

Post a Comment